SIFA YA KWELI INAYOUPENDA MOYO WA MUNGU
MUNGU aliweka nyingi za taratibu za
ibada ya sifa katika Agano la Kale, akachangia sana kwenye kitabu cha
Zaburi, ambacho maneno yake watunzi wengi wa nyimbo wanatumia hadi leo
hii. Hata hivyo, baada ya karne chache kuwa zimepita Mungu ilibidi
awakemee watu wake kupitia Isaya (29:13) kwa kumwabudu kwa midomo wala
si kwa mioyo yao; jambo ambalo hata Yesu alilifanya wakati wa huduma
yake. Miaka 3000 baada ya Daudi ingefaa Kanisa kuyatilia maanani haya
maneno.
Injili ya msalaba ilipoanza kuweka mizizi kwenye makanisa ya ibada ya
sifa ilianza kuleta sura halisi ya uhusiano wetu na Yesu Kristo. Watu wa
Mungu wakaanza kuelewa ya kwamba sifa ya kweli na safi ni ile
iliyoelekezwa kwa Yesu peke yake na ambayo imetoka katika moyo safi.
Jambo lingine tofauti na hilo ni kuutumbuiza mwili tu, muziki mzuri
unaochezwa na wanamuziki stadi! Daudi hasifiwi kwa kuwa alikuwa mtunzi
mzuri wa nyimbo, au kiongozi mzuri wa sifa, bali anafahamika kama mtu
‘aliyeupendeza moyo wa Mungu’! Leo hii, inaonekana ya kwamba watu wengi
wanaojihusisha na sifa na kuabudu wanajitahidi kuiga namna Daudi
alivyotumia vipaji vyake; hawaelewi ya kwamba wanapaswa kuwa na hali ya
moyo aliyokuwa nayo Daudi katika uhusiano wake na Mungu.
Lengo ni Kuabudu
“Kusifu na kuabudu sio njia ya kutafuta kibali kwa Mungu, au hata mbinu
ya kumlazimisha atusikie na kututimizia haja zetu. Kusudi zima la
kuabudu ni kumfanya mtu awe huru kuelezea shukrani zake kwa Mungu kwa
yote aliyomtendea; kuufurahia uwepo Wake na kuukiri ukuu Wake. Muziki na
nyimbo vinapaswa viwe tu njia ya kufanikisha hili lengo – lakini badala
yake vimefanyika kuwa ndilo lengo kuu!” anasema Peter McKenzie,
Mchungaji, Uingereza.
Kama ilivyo katika mambo yaliyo na mchanganyiko wa misisimko, vipaji vya
kimwili, kiburi na majivuno, mambo yanavuka mipaka haraka sana.
Makanisa mengine leo hii yana fundisho la muziki na kuabudu, huku
mengine yakisisitiza ‘ubora wa huduma’ kutoka kwa timu ya uimbaji:
mavazi ya kisasa yanayofanana; muziki usiokuwa na dosari yoyote; vyombo
vya kisasa vya bei ghali, n.k., mambo ambayo tunaweza kuyaita ‘matendo,
sheria, na juhudi za kimwili’. Makanisa mengine yana vitengo vya muziki
vyenye uongozi unaojitegemea mbali na uongozi wa kanisa, kwa sababu tu
vinaliingizia kanisa fedha…Iwe ni katika nchi za Ulaya ‘zilizoendelea’
au katika Afrika au Asia, suala la kusifu na kuabudu limechukua mwelekeo
wa aina yake, na linaonekana halina uhusiano na namna Mungu
anavyoliona.
Kwa hivyo, ingawa sifa na kuabudu linaonekana kuwa ni suala la ‘ndani’
la Kanisa – yaani, si jambo la kuuonyeshea ulimwengu – lakini moyo
unaotoa hiyo ibada, nia sahihi, moyo sahihi, na muziki unaotokana na
hayo mambo kwa vyo vyote utauathiri ulimwengu. Wakristo wanafurahia
nyimbo za injili kuwepo kwenye ‘chati’ za miziki ya dunia; Jina la Bwana
linatukanwa kwa kuchezwa kwenye vilabu vya usiku, ambapo vileo, madawa
ya kulevya na uasherati vinaendekezwa; mapigo na midundo ya kidunia, na
mavazi ya kidunia na kucheza dansi vinaendana na maneno matakatifu;
kwenye baadhi ya makanisa ni vigumu kutofautishaa ibada zake na
matamasha ya kidunia, kwani zinaambatana na fataki na vimulimuli; muziki
wa Kikristo wa ‘rock’, kizazi kipya, ku-‘rap’, reggae…ni nini
kitakachofuata? “Ulimwengu umelivamia kanisa”, anasema Miki Hardy. “Ni
muhimu sana viongozi wake waamke na waangalie suala la kusifu na kuabudu
kwa mtazamo tofauti, wa ki-Uungu!”
Kulingana na Moyo wa Mungu
Katika Yohana 4, Yesu anaeleza tutakavyojaliwa kumwabudu Mungu ‘katika
Roho na katika kweli’ kupitia wokovu utakaokuja kwetu sisi, Kanisa.
‘Wakati’ aliozungumzia ni wakati wa kifo chake msalabani, ambacho
kingefungua njia mpya na tofauti ya kumwabudu Mungu katika uhuru na kwa
moyo safi. Kuna gharama iliyolipwa kutuwezesha tumwabudu Muumba wetu kwa
jinsi hii! “Hakuongea na mwanamke Msamaria kama kiongozi wa sifa; bali
alikuwa akiufunua moyo wa Baba kwa Kanisa lake”, anasema Eugene Nyathi –
Mchungaji na Mtunzi wa nyimbo, Zimbabwe.
Yesu alitufundisha kumpenda Mungu kwa nafsi yetu yote. Na ni kwa
kuyafananisha maisha yetu na kuteswa kwake, kifo chake na kufufuka kwake
– injilii ya Msalaba – ndipo tutakapoweza kumwabudu sawasawa na moyo wa
Mungu. “Sifa ya kweli ni matokeo ya maisha yaliyotolewa sadaka kwenye
barabara ya msalaba”, anasema Roland La Hausse – Mzee wa Kanisa,
Mauritius.
Kumpendeza Mungu
Wanamuziki wengi wanaonekana kuchukulia vipaji walivyopewa na Mungu
kama kitu cha kujiletea manufaa na maslahi binafsi na utukufu, huku
wakisahau kuwa, kama ilivyo kwa vipawa vingine vilivyotolewa Kanisani,
hivi vipaji ni kwa ajili ya kuwahimiza watu wamwabudu Mungu. Ni maisha
ya waimbaji yaliyosalimishwa na kutolewa yanayompendeza Mungu na
kufungua mlango kwa ajili ya hicho kipawa kuchukua nafasi yake stahili
Kanisani.
“Nina hakika Bwana hufurahia sauti nzuri…ila ninaamini hufurahia zaidi
sauti mbovu inayotoka katika moyo safi!” anasema Vanessa Fitzroy –
Muimbaji, Mauritius; ambapo anaongeza Jonathan Hett, mcheza violini
kutoka Mauritius: “Nilipojiunga na kikundi cha uimbaji, niligundua
haraka sana ya kuwa jambo la muhimu zaidi halikuwa uwezo wangu; bali ni
maisha yangu yaliyotolewa madhabahuni, katika hiyo wiki!”
Uhusiano Sahihi
Ibada ya kweli si ibada ya Jumapili tu. Wakristo wote wameitwa
wadhihirishe moyo wa sifa kama kielelezo cha imani yao, unaotokana na
shukrani waliyo nayo siku kwa siku. Wakati huo huo, maombi na sifa za
kweli zinakuwa ni madhihirisho ya kile tulichobeba mioyoni mwetu; kama
hakuna kitu, itabidi tuigize. Zaburi za Daudi ni kielelezo cha uhusiano
wake na Mungu. Hakuna eneo la maisha yake lisilokuwa wazi kwa ajili ya
kuguswa na Bwana. Anamwelezea Mungu kuwa ni mwamba wake, ngome yake,
kimbilio lake, msaada wake, nguvu yake…anayesikiliza, na kusikia, kilio
chake na maombi yake. Kutokana na uhusiano wa jinsi hiyo, ni wazi kwamba
Daudi angeweza kuandika na kuimba zaburi za jinsi hiyo.
2 Mambo ya Nyakati inasema: “Na wakati ilipoanza sadaka hiyo ya
kuteketezwa, ukaanza na huo wimbo wa BWANA...” Clara Grant – muimbaji
toka Mauritius, anaelezea kipindi alichopitia cha utupu wa rohoni, na
ugumu wa moyo kwa Bwana: “Niliimba kwa sababu nilifahamu maneno, lakini
kusifu kwangu kulikuwa kumekufa kabisa. Lakini, mara tu niliposalimisha
kila kitu na nikawa tayari kuuchukua msalaba wangu na kumfuata Yesu
katika yale mazingira, sifa ilibubujika kutoka katika roho
iliyopondeka.”
Si kwa Jumapili tu
Kwa maana hiyo, sifa si kijisanduku cha maisha ya Mkristo,
kinachofunguliwa pamoja na timu ya uimbaji Jumapili asubuhi. Ni
udhihirisho wa hali ya juu wa mtu aliyeyasalimisha maisha yake kwa Mungu
kwani inahusisha nafsi yake yote… Kwa kadiri Roho anavyotuongoza, sauti
zetu zinaimba, mikono yetu inapiga makofi, miguu yetu inacheza…
tunapata utoshelevu mwingi katika kukisogelea kiti cha enzi cha Mungu na
uwepo wake. Tunamwabudu Mungu wetu si kupitia uimbaji tu, bali kwa
kusalimisha kwake karama zetu na vipaji vyetu, muda wetu, pesa zetu,
huduma zetu, na maisha yetu kwa ujumla wake wote.
Pale Mungu alipowaletea watu wake ukombozi na ushindi katika Agano la
Kale, nyakati za kipekee za kusifu na kuabudu zilishuhudiwa,
zikidhihirishwa kwa moyo wa furaha, uimbaji na kucheza. Madhihirisho
mengine ya sifa na kuabudu yalitokea walipoletwa kwenye toba; na pia
kila wakati waliposujudu mbele zake katika kumkumbuka kuwa Yeye ni nani…
Mungu Mkuu, Mungu mwenye uwezo na upendo! Kwenye Agano Jipya, kusifu na
kuabudu vinapaswa viwe kwa sababu zizo hizo, na kwa kufuata utaratibu
huo huo, pamoja na kushukuru kutokana na kwamba Yesu, Mwana wa Mungu,
alikuja kuleta wokovu, ukombozi, na ushindi kwa wote wanaomwamini.
Lakini haitoshi tu kujumuika katika kumsifu na kumuabudu Bwana, ikiwa
mioyo yetu haiko sawa kwake na kwa watu wengine.
Tusisahau ya kwamba hakuna jambo tunaloweza kufanya kwa nguvu zetu na
kwa uwezo wetu linalokubalika mbele za Mungu. Ni lazima tuhoji, basi, ni
kwa nini katika mengi ya makanisa leo hii mkazo umewekwa kwa kile
mwanadamu anachoweza kufanya kwa kipaji chake cha uimbaji na ni kiasi
gani cha uwezo wake kilichoelekezwa katika kutumbuiza. Dhana ya ‘ubora
wa huduma’ pia imeenea, kana kwamba tunaweza tukampendeza Mungu kwa
kwaya zetu zenye mavazi mazuri, vyombo, na kadhalika…
Yesu huangalia Moyo
Jocelyn Sery – Mzee wa Kanisa na mtunzi wa nyimbo kutoka St. Pierre, La
Reunion, anasema: “Nilitumia miaka mingi yenye kukatisha tamaa
nikijitahidi kutumia kanuni za kibiblia katika sifa, bila kuyafananisha
maisha yangu kikamilifu na msalaba wa Kristo. Kabla ya kuja huo ufunuo,
na msalaba kuanza kufunua nilichokuwa nacho moyoni mwangu – jinsi mwili
wangu ulivyokuwa umeunda mbinu za kuficha uongo ulioyatawala maisha
yangu – nilikuwa sielewi kabisa Yesu alichomaanisha aliposema
tutamwabudu katika Roho na katika kweli. Nikaona jinsi sheria, au mkono
wa mwanadamu, ulivyokuwa umeikanyagia chini neema ya Mungu. Nilimwabudu
Mungu kwa kanuni za kibinadamu; lakini, machoni pa Mungu, sifa yangu
ilionekana ya uongo. Amosi 5:23-24 na 6:5 inatuonyesha jinsi Mungu
asivyoangalia vipaji vyetu vya uimbaji. Ni kwa sababu Yeye husikia mambo
ambayo sauti zetu haziyatamki. Yeye huona mambo yote tunayojaribu
kuficha…Kwa sababu ushirika wa Mungu si pamoja na miili yetu, bali na
mioyo yetu!”
Sifa iliyonajisiwa na Ulimwengu
Katika makanisa mengi na matamasha, ibada ya sifa imechanganyikana na
roho ya dunia kiasi kwamba ni vigumu kutenga ya Mungu na ya dunia.
Uongozi wa makanisa umeruhusu kughoshi ili ‘kuwaweka vijana kanisani’.
Hata kucheza kuliomo katika mengi ya makanisa si matokeo au matunda ya
ushindi, kama Daudi alivyocheza mbele za Bwana wakati wa kulileta
sanduku la agano kwenye mji wa Mungu. Leo hii Wakristo hawahitaji
ushindi au kumbukumbu ya kile Bwana alichofanya ili waenende kana kwamba
wako kwenye vilabu vya usiku… Kucheza, kurukaruka na kuchezesha miili
yao kwa kufuata miziki ya kidunia na yenye kusisimua hisia kwa kiwango
cha hali ya juu. Mungu na atusaidie! “Wanafanya mambo kanisani ambayo
wangetamani kufanya duniani!” anasema Miki Hardy.
Malengo ya Kidunia
Joelle Atisse – Mtunzi wa nyimbo, Curepipe, Mauritius, anasema:
“Nakumbuka juhudi zangu za kutaka kufanya vizuri, nikijua watu
wangesifia uimbaji wangu... Ndani mwangu nilikuwa na makusudi na malengo
ya kuwa mtu ambaye angependwa na mwenye kufurahisha machoni pa watu
wote... Lakini, kadiri nilivyozidi kusikiliza Injili ya Msalaba, haya
makusudi yote yakadondoka, moja baada ya lingine; Bwana ananielekezea
kioo cha kunionyesha jinsi ninavyokuwa dhaifu wakati siubebi msalaba.
Naona waziwazi kwamba roho ya dunia inauteka moyo wa mwanadamu na
kumpeleka mbali kwa muziki wa giza unaovutia tu hisia zake. Unaweza
ukaathiri au kuambukiza ujumbe wowote mzuri au mbaya kwa njia ya maneno
na nyimbo. Nyimbo zenye upako na zilizovuviwa Roho wa Mungu zinapoimbwa,
Roho wa Mungu anatembea na anagusa, anaponya, anavunja, anakemea na
kuifariji mioyo. Kwa upande mwingine, nyimbo za kidunia zinatoa mwanya
kwa Shetani ambapo maisha ya watu yanapata athari mbaya na hatimaye
kuharibiwa. Mimi natamani zaidi na zaidi Roho aniongoze. Nimekuja
kugundua ya kuwa pamoja na udhaifu wangu na kasoro zangu, Bwana
anapendezwa na moyo mnyofu usiotaka kuchanganya, bali unaotaka
kujisalimisha kikamilifu kwake.”
Kile Yesu alichonena katika Yohana 4 ni ibada yenye uhalisia na ya kweli
itokayo katika vina vya mioyo yetu na iliyomwelekea Kristo tu. Hili
linadhihirisha jinsi moyo wa kiongozi wa sifa unavyopaswa kuwa msafi,
kwa sababu alichobeba ndicho atakacholivuvia Kanisa.
Udhihirisho wa Moyo Wangu
Eugene Nyathi – Mzee wa Kanisa na mtunzi wa nyimbo, Zimbabwe, anasema:
“Kwa sababu hii, sifa haianzi pale tunapoimba wimbo. Uimbaji ni
udhihirisho wa moyo wangu kwa Mungu. Mungu huangalia hali ya moyo wangu
zaidi ya maneno ninayoimba. Ninawafahamu watu wengi wa Mungu wenye sauti
zisizovutia. Hebu fikiri ingekuwa sifa ingepimwa kwa aina ya sauti.
Ingekuwa hivyo, basi wengi wasingemwabudu Mungu... hakika si machoni
petu! Mwimbaji mwenye sauti mbaya anaweza asivutie sana, lakini huyo mtu
anaweza akawa mbele ya kiti cha enzi cha Mungu kwa wakati huo,
akitazamana na Mungu uso kwa uso. Ila kwako wewe, kile wanachoimba
kinaonekana kutokukubalika kwa kuwa hakina ‘mvuto’. Lakini kumbuka Mungu
huangalia mioyo. Ni zaidi ya muziki au nyimbo nzuri, au uimbaji
mzuri... ni maisha yako!”
Kutokana na shuhuda zote hizi, tunaona ya kuwa moyo sahihi na ufahamu
sahihi juu ya uhuru tulio nao katika Kristo ndio msingi wa yote
tunayofanya kuhusiana na sifa. Kama mtu mmoja alivyosema: “Muziki si
sifa, ila sifa inaweza ikawa muziki!”
Kuabudu kwa njia ya Ufunuo
Jean-Jacques Fabien, Kiongozi wa sifa na mtunzi wa nyimbo toka Curepipe,
Mauritius, anasema: “Ni sharti pia kuwepo na ufunuo wa neema ya Mungu
ili tumwabudu katika uhuru na si kwa kanuni. Huu ufunuo unaweza
ukadhihirika na kukua tu mioyoni mwetu tunapohubiriwa injili ya
Msalaba wa Yesu; msalaba ukiwa ni mahali na muda ambapo mabadiliko
yalifanyika katika namna ya kuweza kuufurahia ushirika na maisha yetu
naye... si tena katika roho, au kanuni, au sheria yeyote ile ya Agano la
Kale, bali katika neema yake. Ninaamini tumeitiwa uhuru wa kuyaishi
maisha ya ufunuo wa msalaba na wa neema ya Mungu kusudi tutembee katika
ngazi ya juu zaidi ya sifa... sifa ya kweli inayompendeza Mungu. Kwangu
mimi, sifa ina uhusiano na maisha yangu katika ujumla wake, na si
muziki!”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni