Mungu Amwonyesha Nabeel Njia ya Kweli Kati ya Uislamu na Ukristo - Sehemu ya 2
Katika sehemu ya kwanza ya ushuhuda huu wa Nabeel,
aliyekuwa Mwislamu kisha akakutana na Bwana Yesu na kupokea wokovu, tuliona
jinsi ambavyo alimwomba Mungu ampe maono yatakayomwonyesha imani ya kweli.
Alionyeshwa misalaba kwenye maono lakini yeye akasema labda ni macho yake tu
yamemchezea mchezo. Kwa hiyo, alimwomba tena Mungu kwamba, kama
yale maono yalitoka kwake, basi ayathibitishe kwa ndoto. Je, Mungu alifanya
nini? Tafadhali endelea kusoma sehemu hii ya pili.
…………………………………
Mungu alinipatia ndoto ile kwa uwazi sana kiasi kwamba sikuwa na ulazima wa
kuitafsiri. Lakini ilikuwa wazi hata zaidi kuliko nilivyotarajia. Saa chache
baadaye niliwasiliana na David na kumwambia kuwa nimeota hivi na hivi.
David aliniambia, “Sina ulazima wa kutoa maoni yangu juu
ya hilo. Kila
kitu kiko kwenye Biblia.”
Nikasema, “Unasemaje?”
Akasema, “Nenda kwenye Luka 13.”
Nilienda kwenye Luka 13 mstari wa 22 hadi 29. Niliposoma
nikakuta kumeandikwa kuhusu kuingia kwenye Ufalme wa Mungu, na Kristo akasema
kwamba, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza. Jitahidini kuingia kupitia
mlango mwembamba. Na watu watakuwa wamesimama kwenye mlango huo wakibisha hodi.
Na hicho hasa ndicho kilichotokea kwenye ndoto yangu.
Nilikuwa kwenye huo mlango ambao ulikuwa haujafungwa bado. Fursa ya mimi
kuingia humo kwenye kushiriki sherehe ile ilikuwa bado ipo. Nilichotakiwa tu
kufanya ni kukubali mwito.
Papo hapo nilitambua kile ninachotakiwa kufanya. Nilibaini
kwamba Uislamu haukuwa ile kweli. Mungu alikuwa ananivuta nitoke humo. Japokuwa
mimi nilikuwa siko tayari, lakini aliendelea kunivuta.
Ikawa ni kama naingia
kwenye majonzi na msiba. Nilikuwa nalia ninapoelekea shuleni. Siku moja
nikamwambia Mungu, “Mungu, nipe tu siku chache ili niomboleze. Nahitahi
kuomboleza, maana nina watu wengi ambao nitawapoteza.”
Niliporudi kwenye chumba changu, nilifungua Quran na
hakukuwa na kitu cha kunisaidia humo. Nilifungua Biblia kwenye kitabu cha
Mathayo, na kabla hata sijamaliza sura ya 5, nikakutana na maneno: Heri wenye
huzuni; maana maana hao watafarijika. Na nikasoma Ayubu, na uchungu wote
niliokuwa nao ukaisha. Lakini kwenye Quran sikuwa na msaada wowote! Quran
ilikuwa ikinipa tu maelezo ya mambo ya zamani, lakini hakuna kitu cha kunisaida
sasa. Hakuna kabisa! Lakini kila mara nilipofungua Biblia, msaada ulikuwa pale.
Ninamwomba Mungu kitu halafu namwuliza, “Nitajuaje kuwa
nitapata hiki?” Kisha ninafungua 1 Yohana 5:14-15 na inasema: Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa,
tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama
tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja
tulizomwomba – maana tunaamini mioyoni mwetu kwamba Yesu ni Bwana. Niliamini
moyoni mwangu kwamba Kristo ni Bwana lakini sikuwa nimekiri.
Warumi 10 nayo inasema kitu hichohicho. Inasema: Kwa
sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni
mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Na mimi nilikuwa sijafanya
hivyo.
Kisha akili yangu ilifunguka nilipokuwa nasoma kwenye
Mathayo, inaposema: Bali
mtu yeyote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu
aliye mbinguni. Na pia inasema: Bali, kila mtu
atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Ilikuwa ni hapo ndipo sikuweza kumkana Kristo tena!
Sikuweza kumkana Mungu tena! Sikuendelea kushikilia tena maisha yangu na
mitazamo yangu ambayo nilikuwa nayo, si kwa sababu niliamini, bali kwa vile tu
nilizaliwa na kukua katika hiyo. Nilianza kutambua kwamba ile haikuwa kweli na
nikaanza kumkubali Kristo maishani mwangu.
Nilimwomba Roho Mtakatifu anibadilishe maisha yangu. Na
baada ya kuomba sala ile, ulimwengu wote ukawa tofauti. Niliposema maneno yale,
nilishtushwa kana kwamba nimepigwa shoti ya umeme. Yalikuwa ni maneno tu,
lakini yalikuwa ni maombi ambayo Mungu aliyatimiza.
Na Roho Mtakatifu alipoingia ndani yangu wakati huo,
nikawa nimeshikwa kwa dakika zipatazo kumi kama
mtu aliyenaswa na umeme. Kwa dakika kumi nilikuwa siwezi hata kusogea! Na pale
nilipoweza kusogea, niliutazama ulimwengu ulionizunguka na ulikuwa mzuri sana! Kulikuwa kumejaa
matumaini; kulikuwa kumejaa maana! Nilitambua nini maana ya maisha.
Si suala tu la kuishi kama
mtu mwema - ni kweli unatakiwa kufanya
hivyo. Lakini lengo la msingi kabisa la maisha yetu ni kumsifu na kumwabudu
Mungu mmoja wa kweli, aliyekuja kwenye ulimwengu huu, na kufa kwa ajili ya
dhambi zetu ili tuweze kuona jinsi anavyotujali; ili tuweze kumwabudu Yeye
kikamilifu, kwa furaha – kama ambavyo Paulo
anasema kwenye Wafilipi: Furahini wakati wote – maana Mungu yuko karibu.
Maisha yangu yalikuwa na maana sasa, maana nilikuwa sasa
naweza kwenda nje na kuhubiri. Haikuwa ni kukaa tu na kusema, “Kila mtu
anayefanya mema, atakwenda mbinguni.” Hapana! Sasa kulikuwa na suala la kwamba,
watu wanahitaji kujua Mungu ni nani; na nini amefanya. Watu wanahitaji kujua
nafasi yetu ni nini kwa habari ya uhusiano wetu na Mungu; wanatakiwa kujua kuwa
tunatakiwa kumwabudu Mungu mmoja wa kweli na Mwanawe, Yesu Kristo ambaye
alikuja kufa kwa ajili ya dhabi zetu.
Tunatakiwa kuwaambia watu kuwa, ndiyo, Mungu ni mmoja.
Hata hivyo, Yeye ni mmoja katika Utatu, na Utatu katika mmoja. Iwe tunaweza
kuelewa hilo au
hatuwezi, ni jambo lililo nje ya uwezo wetu. Si lazima tuelewe. Cha msingi ni
kujua tu kuwa Yesu ni Mungu; kwamba Mungu aliamua kuja duniani kama mtu.
Waislamu wanaona kuwa hilo haliwezekani. Hakuna sababu ya hilo kutowezekana. Mungu
anaweza kuamua kuja duniani kama mtu.
Nionyeshe kwenye Quran panaposema kwamba Mungu hawezi. Badala yake, Quran
inaonyesha kuwa Mungu anaweza kufanya chochote atakacho.
Siku ya mwisho, ya kiama kama
Quran inavyosema, tutahukumiwa. Hakuna mtu anayeweza kwenda mbinguni, hata
Waislamu, kwa juhudi zake mwenyewe. Ni lazima iwe kwa neema ya Mungu. Hata
mtume wa Uislamu alisema watu waombe msamaha kwa Mungu mara nyingi kwa siku
maana hajui kama ataingia mbinguni au la. Ni
kwa neema ya Mungu pekee.
Hiyo neema sasa, ambayo hata Waislamu nao wanaitegemea
siku ya mwisho ili kuingia mbinguni, ni neema ileile ambayo Wakristo
wanaitegemea. Tofauti tu ni kwamba, Wakristo wanaamini kuwa neema hiyo tayari
ilishatolewa kwenye msalaba miaka 2000 iliyopita Mungu aliitoa hiyo neema kwa
ajili yetu. Ni neema ileile, si nyingine tofauti, tunatakiwa tu kutafuta kwa
mioyo yetu yote. Naamini kwamba yeyote anayemwomba Mungu kwa moyo ulio wazi
aonyeshwe kweli, ataonyeshwa kweli!
…………………………………..
Mpendwa msomaji, umemsikia Nabeel jinsi alivyokuwa na
shauku ya kumjua Mungu wa kweli. Mungu si kiziwi. Yeye hujibu haja na shauku za
mioyo yetu za kutaka kumjua na kumpendeza. Kwa nini usimwambie akuonyeshe njia
ya kweli? Yesu ni njia, kweli, na uzima. Hakuna mtu anayeweza kwenda mbinguni –
hata kama ni Mkristo – kama hajamkaribisha
Yesu kuwa Bwana na Mwokozi maishani mwake na moyoni mwake.
Tafakari.
Jihoji.
Chunguza mambo.
Kweli imo ndani yako.
2 comments:
Hakika Mungu anatenda mema na
kutuonyesha njia ya kweli bila kumkaribisha Yesu Kristo kuwa bwana na mokozi wa
maisha yako kwamwe hauwezi kuona ufalme wa Mungu
Ni kweli kabisa Stepha.
Mwanadamu alifukuzwa Edeni kwa sababu ya dhambi. Hakuna mwanadamu asiye na
dhambi. Hiyo ina maana kuwa hakuna mwanadamu anayeweza kuingia mbinguni kwa
jitihada za kutunza sheria za Mungu. Hiyo maana yake pia ni kuwa, kuingia
mbinguni ni LAZIMA iwe ni kwa njia nyingine. Yesu ndiye njia hiyo. Yesu ni
NEEMA ya Mungu kwa mwanadamu. Kumwamini Yesu ndiyo njia PEKEE ya kuingia
mbinguni. Ubarikiwe na Bwana.