Ijumaa, 1 Novemba 2013

KUOKOLEWA KWA NEEMA

KUOKOLEWA KWA NEEMA

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe       

Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe        
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Somo:  Kuokolewa Kwa Neema
Watu wanaosema kwamba haiwezekani kuokoka duniani, wanasema hivyo, kwa sababu hawajui kwamba tunaokolewa kwa neema tu!  Biblia inasema katika WAEFESO 2:8-9, “kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu (yaani zawadi kutoka kwa Mungu); wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”.  Tunasoma pia katika YOHANA 1:16, Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema”.  Iko siri kubwa iliyofichika katika maana ya neno, “Neema”.Kama sisi sote tungefahamu jinsi tunavyookolewa kwa neema, na jinsi tunavyopokea neema juu ya neema; kwa hakika, hakuna mtu hata mmoja ambaye angekwenda kwenye mateso ya moto wa milele. Wote tungekwenda mbinguni kirahisi sana, kwa kuwa tunaingia mbinguni, kwa neema tu; na Shetani asingepata mtu wa kukaa naye motoni, ila malaika zake tu, maana moto wa milele haukutengenezwa kwa  ajili ya wanadamu, bali ulitengenezwa kwa ajili ya Shetani na malaika zake tu (MATHAYO 25:41).
Kwa bahati mbaya, nyakati hizi tunazoishi duniani mafundisho juu ya neema, yamekuwa nadra sana kupatikana katika majengo ya ibada.  Watu wanaingia katika majengo ya ibada, miaka nenda, miaka rudi, bila kufahamu maana ya neema.  Haikuwa hivi wakati Mtume Paulo alipokuwa akitenda kazi duniani.  Nyakati za Mtume Paulo, karibu kila mtu alifahamu maana ya Neema.  Ndiyo maana ulimwengu wote ulipinduliwa juu chini (MATENDO 17:6), na Shetani akawa katika hatihati ya kukosa wafuasi.    
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .                   Iko siri kubwa iliyofichika katika maana ya neno, “Neema”
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Wako watu wengi leo ambao wanaimba wimbo maarufu, “Neema, Neema, Neema, imefunuliwa”, lakina ukiwauliza ni nini maana ya neema, hawawezi kukujibu.  Wako watu wengine ambano hukariri, na kusema kwa ufundi mkubwa sala ya Neema, “Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nasi sote, sasa na hata milele. Amen”  (2 WAKORINTHO 13:14).  Hawa nao ukiwauliza ni nini maana ya “Neema”, utashangaa kuona kwamba wengi kati yao, hawafahamu maana ya neema.  Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.  Ndiyo maana, mpendwa msomaji, Mungu, kwa makusudi kabisa, amekuletea “note” hii, ili tupate kujifunza kwa pamoja, maana ya neema, kwa jinsi ileile watu walivyojifunza, wakati wa Mtume Paulo.  Ukisoma “note” hii hadi mwisho, hutakuwa jinsi ulivyo katika Jina la Yesu!
Nini basi, maana ya Neema?  Ziko aina mbili za neema tunazozipokea kutoka kwa Mungu.  Ndiyo maana tunasoma katika YOHANA 1:16, kwamba tunapokea “Neema juu ya Neema”.  Aina ya kwanza ya Neema, ni upendeleo wa kuchaguliwa bila kuwa na sifa zinazostahili.  Kwa kawaida, nafasi ya kazi nzuri, yenye mshahara mzuri inapotokea, mwajiri hutangaza nafasi ya kazi hiyo, na kuelezea sifa za mtu anayetakiwa kuajiriwa.  Kwa mfano, mwajiri anaweza kusema, “Anatakiwa mtu aliye na digrii ya uchumi, na mwenye uzoefu wa kazi hii kwa muda usiopungua miaka mitano.  Awe na umri wa miaka 40 au zaidi, na mwenye haiba nzuri.  Mtu mwenye uwezo wa kutumia kompyuta, atafikiriwa zaidi”.  Baada ya watu kusoma au kusikia tangazo hili la kazi, wengi hutuma maombi ya kazi.  Hatimaye watu mia mbili au zaidi wanaweza kuchaguliwa kwenda kwenye mahojiano au “interview”, na kati yao mtu mmoja tu mwenye sifa za hali ya juu kuliko wengine wote, ndiye atakayechaguliwa.
Sasa basi, kuokolewa na kuhesabiwa haki ya kuingia mbinguni, ni kitu cha thamani kuliko kazi yoyote ile, hata ingekuwa na mshahara mkubwa kiasi gani.  Hata tukiwa na kazi nzuri yenye mshahara mkubwa, siku moja tutaiaga dunia hii, na kuiacha; na tukiwa tumeishi dhambini, mshahara, wetu utakuwa mauti ya milele, yaani kutupwa katika mateso ya moto wa milele (WARUMI 6:23).  Lakini ikiwa tumeishi maisha yanayompendeza Mungu, tutaokolewa kutoka katika mateso hayo, na kuishi na Mungu mbinguni, kwenye raha isiyo kifani; milele na milele.  Sasa basi, Mungu anachaguaje watu wa kuingia mbinguni?  Je, anaangalia sifa au matendo yao?  Jibu ni la. Tulisoma, na tunasoma tena katika WAEFESO 2:8-9, “Kwa maana mmeokolewa kwa neema,…….. wala si kwa matendo”.  Hatuokolewi kutokana na matendo yetu tuliyoyafanya kamwe.
Kutokana na matendo yake, hakuna mwanadamu yeyote mwenye haki, mbele za Mungu (WARUMI 3:20).  Tangu mwanzo kabisa mwanadamu amekuwa akimhuzunisha Mungu kwa maovu yake kiasi ya kumfanya Mungu kughairi kwa nini amewaumba wanadamu.  Katika MWANZO 6:5-7, BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.  Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.  BWANA akasema, Nitamfutilia mbali  mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani, kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya”.  Baada ya maneno haya, Mungu aliwaangamiza wanadamu wote kwa Gharika, kasoro watu wanane tu, Nuhu na jamaa yake.  Wakati wa Musa, vivyohivyo, Mungu alitaka pia kufuta kabisa kizazi cha Waisraeli, na kubaki na Musa peke yake; kama siyo maombi ya Musa (HESABU 14:11-20). Katika vizazi vyote, Mungu anatoa ripoti ifuatayo juu ya maisha ya wanadamu, “Wote wamepotea, wameoza wote pia; hakuna mtenda mema la! hata mmoja”  (WARUMI 3:12).  Katika wanadamu wote, waliowahi kuishi duniani, ni Yesu Kristo tu aliyeishi duniani bila kufanya dhambi. 
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

       Ni Yesu Kristo tu aliyeishi duniani, bila kufanya dhambi
. . . . .. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .
Siku zote, Yesu Kristo alifanya yale yanayompendeza Mungu (YOHANA 8:29).  Alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote bila kutenda dhambi hata moja (WAEBRANIA 5:14-15).  Huyu pekee ndiye Mungu anayemtaja akisema, “Huyu, ni Mwanangu mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (MATHAYO 3:17).  Sasa basi, sisi wanadamu tunaokolewa siyo kutokana na matendo yetu bali kutokana na matendo ya Yesu Kristo.  Tunachotakiwa kukifanya ni kumwamini Yesu tu na kuifurahia kazi ile aliyoifanya msalabani, pale alipochukua adhabu iliyomstahili Baraba, mfungwa mashuhuri.  Baraba akafunguliwa na Yesu akachukua adhabu yake ya kifo (MATHAYO 27:16-17,  20-26).  Sisi nasi ni wahalifu, wenye dhambi kama Baraba, na tunaokolewa kutoka katika adhabu ya mauti ya milele, yaani mateso ya moto wa milele, kwa imani tu, katika adhabu aliyoichukua Yesu kwa niaba yetu.
Tungeweza kusema kwamba  Baraba, mtu mhalifu, aliwekwa huru au aliokolewa katika adhabu ya kifo kwa neema tu!  Hakustahili!  Kutokana na Yesu kuchukua adhabu hiyo, Baraba akawa huru.  Vivyo hivyo, kutokana na Yesu kumpendeza Mungu sikuzote, sisi nasi tunahesabiwa haki ya kuingia mbinguni alikokwenda, kwa imani tu katika Yeye!  Kazi njema aliyoifanya Yesu, imetupa kuirithi mbingu aliyokwenda bila sisi kuifanya.  Ni kama jinsi ambavyo katika mambo ya dunia, bondia anavyopigana ulingoni kwa shida kubwa, na kisha akishinda na kupewa mamilioni ya fedha; mke wake aliyebaki nyumbani bila kupigana, naye anakuwa milionea!  Hii ndiyo Neema!  Yesu Kristo, ndiye aliyepigana na Shetani na kumshinda pale alipomjaribu kufanya dhambi, na sisi tunahesabiwa kushinda katika Yeye Yesu, kwa imani tu!  Ndiyo maana Biblia inasema katika WAEFESO 2:8-9, Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu (Zawadi ya Mungu), wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”.
Kwa hiyo tunachotakiwa kukifanya, ili tuokolewe, ni rahisi sana.  Tunatakiwa kutubu dhambi zetu kwa kumaanisha kuziacha, na kwa imani tu, katika Yesu Kristo, tunahesabiwa mara moja haki ya kuingia mbinguni.  Hiyo ndiyo neema ya Kwanza.  Aina ya pili ya Neema, ni msaada utokao mbinguni, wa kutuwezesha kufanya mapenzi ya Mungu.  Kama tulivyoona, hatuokolewi kutokana na kujitahidi kufanya hili au lile, bali ni kutokana na kazi aliyoifanya Yesu, siyo sisi.  Vivyo hivyo, kutokana na upendo wa Mungu, Mungu anajua pia kwamba hatuwezi kufanya mapenzi yake mpaka atupe msaada wa kutuwezesha kufanya hivyo.  Biblia inasema katika TITO 2:11-12, “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi na haki, na utauwa (utakatifu), katika ulimwengu huu wa sasa”. 
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .                      Bondia akishinda na kuwa tajiri, mkewe naye hutajirika bila kupigana
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Mtu anapofundishwa kuendesha gari, kwa lugha nyingine, huwa amewezeshwa kuendesha gari. Vivyo hivyo, Neno la Mungu linaposema kwamba neema iliyofunuliwa ndiyo inayotufundisha kuishi maisha ya utakatifu katika ulimwengu huu wa sasa, maana yake neema ya Mungu, ndiyo inayotuwezesha kuishi maisha ya utakatifu.  Maisha ya wokovu ni ya kuwezeshwa kufanya mapenzi ya Mungu, siyo kufanya mapenzi ya Mungu kwa kujitahidi kwa nguvu zetu.  Biblia inasema katika WAKOLOSAI 1:10-11, “Mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkiwezeshwa kwa uwezo wote, kwa kadiri ya nguvu ya utukufu wake…..”  Tunayaweza yote katika Yeye Yesu atutiaye nguvu (WAFILIPI 4:13).  Nguvu hii ndiyo Neema ya pili.  Baada ya kuokolewa, tunawezeshwa kufanya mapenzi ya Mungu.  Tunachotakiwa kufanya, kwa kila mapenzi ya Mungu tunayoelekezwa kuyafanya katika Neno lake, tunakikaribia kiti cha neema cha Mungu na kuomba neema au msaada wa kutusaidia kufanya mapenzi yake (WAEBRANIA 4:16).
Mpendwa msomaji, unaona sasa!  Hakuna haja ya kusema, “Hivi kweli nitaweza kushinda dhambi duniani?  Hivi kweli maisha ya wokovu nitayaweza?”  Ni Neema juu ya Neema.  Unalotakiwa kufanya ni kutubu dhambi zako tu kwa kumaanisha kuziacha; kwa imani tu, na mengine yanayofuata mwachie Yesu; na leo hii utashangaa kuona  maisha yako yamebadilika ghafla na kwa urahisi utaona unaweza kufanya mapenzi ya Mungu, bila jitihada za kibinadamu.  Je, uko tayari kutubu dhambi zako?  Najua uko tayari.  Basi sema hivi, Mungu wangu, natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha kuanzia leo.  Asante kwa neema yako ambayo kwa hiyo tunaokolewa kutokana na kazi aliyoifanya Yesu. Niokoe sasa na kunipa neema ya kufanya mapenzi yako kuanzia sasa na wakati wote ujao.  Asante kwa kuniokoa katika Jina la Yesu. Amen”.  Ili uzidi kuukulia wokovu ulioupokea leo, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . .

Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook, Twitter, n.k,  kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “note” hii, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.
                                                         UBARIKIWE NA BWANA YESU!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni