Ijumaa, 1 Novemba 2013

BALAA, LAANA NA MIKOSI YA KIFAMILIA.

BALAA, LAANA NA MIKOSI YA KIFAMILIA.

Na Mchungaji Josephat Gwajima

Mara nyingi unapoenda hospitali, daktari huwa anauliza kama kuna mtu katika ukoo wako, ana historia ya tatizo hilo na jibu lako humsaidia kujua tatizo lako kwa undani. Vivyo hivyo laana, mikosi na balaa vinaweza kufuata familia yako kama zilivyo baraka pia.

Ndio maana watoto wengi wa viongozi serikali huishia kuwa viongozi, na watoto wengi wa maskini hujikuta wanaishia kuwa katika umaskini zaidi, ni ukweli ulio dhahiri kuwa kilichotendwa na baba huwa kinashuka hadi kwa watoto wake. Ukisoma katika Mithali 13: 22 "Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki." Pia, Zaburi 37:25 "Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula."

Adamu na Hawa walipotenda dhambi, hukumu kwa mwanamke ilikuwa hivi, Mwanzo 3:15, Mungu aliweka uadui kati ya uzao wa mwanamke na uzao wa nyoka. Kwanini unafikiri Mungu aliweka uadui hata kwa watu ambao hawakuhusika? Jibu ni kuwa yaliyotendwa na wazazi au mababu wa ukoo yana matokeo sana katika maisha ya mtu ya leo. 2Timotheo 1:3-5 "...5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo." Kumbe kuna uwezekano wa tabia ya mtu kuunganishwa na familia au ukoo wake. Kama imani yaweza kusafiri kiukoo, vivyo hivyo na tabia ya kutokuamini au uovu mwingine waweza kusafiri kutoka kwa mtu kizazi kimoja hadi kingine.

Ndio maana inawezekana, mtu akajikuta anafanya tabia fulani, na ingawa haipendi lakini anaendelea kuifanya kumbe ni kwasababu ya ukoo wake. 1Petro 1:18-19 Waweza kuumkuta mtu mwongo, mwizi, mzinzi, mchoyo, mbisho kumbe ni kwasababu ya tabia za kurithi ambazo zinatokana na laana za familia. Kuna uwezekano mtu akajikuta hana ndoa ya kudumu, kumbe ni kutokana na laana iliyo katika ukoo.

Ni muhimu kumjua adui unayepambana naye, watu wengi sana wanajikuta wanapambana na adui wasiyemjua huku wakidhani wako sahihi, na mwisho hujikuta wana bidii yao haizai matunda, kumbe ni matokeo ya kupambana na adui usiyemjua. Huwezi kushindana na shetani bilankujua mbinu zake "watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa."

Jambo lingine la Muhimu, maamuzi yoyote unayoyafanya leo yana matokeo katika maisha yako na ya uzao wako. Ndio maana wana wa Israeli walipokuwa wanaingia katika nchi ya ahadi Yoshua aliwaambia, "chagueni hivi leo mtakaye mtumikia" uchaguzi unaoufanya leo una matokeo mazuri au mabaya katika maisha yako.

Biblia inasema kila andiko lenye pumzi ya Bwana lafaa kwa mafundisho, kwasababu hiyo tunaweza kujifunza kitu kutoka katika maisha ya baba wa Imani, Ibrahimu. Mwanzo (11:29-30), ibrahimu alikuwa hazai maana Sara alikuwa tasa, tunaona pia mwanaye Isaka naye akawa na tatizo hilohilo la kukosa mtoto kwa mkewe Rebeka (mwanzo 25:21); na jambo hilo halikuishia hapo kwani na Yakobo alipatwa na tatizo hilohilo.

Pia, kwa namna hiyihiyo ukifanya yaliyo mema mbele za Mungu, baraka zako hufuatana na uzao wako. Tunaona jambo hilo kuwa, baraka za Ibarahimu ziliweza kufuatana na uzao wake (Mwanzo 30:1-6; 13:15; 17:7-10) ahadi za Ibrahimu hazikuishia kwake tu bali zilipitiliza hadi kwa uzao wake. Kumbe baraka zaweza kusafiri kutoka kwa mababu hadi wabibi, vivyohivyo laana zaweza kusafiri kutoka kwa kizazi kimoja hadi kizazi kingine. Ndio maana hata Yoabu alipomuua Abneri, ambaye alikuwa awali amesamehewa na Mfalme Daudi, ile laana ilifika hadi kwa uzao wake.

Utajifunza pia kwa habari ya Yesu, walipotaka kumuua, wayahudi walitamka wazi kuwa "25 Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu." Mathayo 27:24-26 wayahudi walijua ukweli huu kuwa laana zaweza pita kutoka uzao mboja wa uovu hadi mwingine, kwasababu hiyo inawezekana unaishi katika mateso leo kwasababu ya mambo yaliyopita huko nyuma.

Mungu hapendi kuwatesa wanadamu wala kuwahuzunisha (Maombolezo 3:33). Lazima usimame kinyume na kila laana katika familia yako na katika maisha yako, jitenge na kila laana za kutoka kwa familia au ukoo wako. Balaa, laana na mikosi ya familia yako na ivunjike katika jina la Yesu Kristo.


Na Mchungaji Josephat Gwajima 

Maoni 1 :

  1. Bwana abariki somo hili!! Nimejifunza Kitu kikubwa Ahsanteee saaana

    JibuFuta