NILIKUTANA NA BWANA YESU GEREZANI NA NDIO UKAWA MWISHO WA KUUZA MADAWA YA KULEVYA
Aokoka na sasa anahubiri Injili
Mchungaji Donald Mwakisambwe wa kanisa la
Kipendekoste la Kiinjili Tanzania, kwenye ofisi za gazeti hili wakati
akitoa ushuhuda wa kufanya biashara haramu ya madawa ya kulevya.PICHA:
TRYPHONE
Akizungumza katika mahojiano maalumu na NIPASHE Jumamosi jana, Mwakisambwe alisema alianza biashara ya unga mwaka 1990 na kuifanya kwa miaka 10, akisafirisha dawa kwa maelfu ya wateja walioko Afrika, Asia, Ulaya na Amerika. Alisema katika kutimiza azma hiyo, alitumia pasi za kusafiria za mataifa mbalimbali zenye majina tofauti, zikimuonyesha kuwa ni raia wa Msumbiji, Tanzania, Kenya, Namibia, Afrika Kusini na Namibia.
Alieleza kuwa, kumiliki pasi hizo kulilenga kuficha wanausalama wasimgundue kuwa ni ‘mzungu wa unga’ aliyekuwa anasafiri nchi mbalimbali duniani ndiyo maana kila alipomaliza mzunguko aliziharibu pasi hizo . Alisema mwaka 1999, Yesu Kristo, alimtokea akiwa rumande kwenye gereza la Industrial Area jijini Nairobi, baada ya kuwasili Kenya akitokea Karachi, Pakistani akiwa na karibu kilo moja ya kete za heroin tumboni.
Mwakisambwe alisema alipotua Nairobi, alikamatwa na maofisa wa polisi kadhaa waliomueleza kuwa ni muuza unga wa kimataifa na kuwekwa chini ya ulinzi kwenye kizuizi cha Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta. “Nilikuwa na pasi ya Msumbiji yenye jina la Danilo Silva Jalla, licha ya kwamba ni Mtanzania”,anasema.
Anaongeza kusema kuwa ili kupata pasi hizo, alibadilishwa sura halisi kwa kujiwekea ndevu za bandia, nyusi na nywele nyingi zilizompa sura tofauti na muonekano mpya kila alipouhitaji. Alisema pasi hizo zilikuwa zikitengenezwa na magenge ya wanaojihusisha na madawa hayo ambao wapo kila mahali na wamewekwa mahsusi kufanikisha usambazaji wa mihadarati kila sehemu inapohitajika.
Alisema hata hapa Tanzania, kuna magenge hayo ya ‘mafia’ na mtandao huo unashirikiana na maofisa wa Idara ya Uhamiaji wasio waaminifu. Mchungaji Mwakisambwe alisema kupitia biashara hiyo, alijenga nyumba kadhaa zilizoko Dar es Salaam na Mbeya pia alikuwa na utajiri mkubwa wa magari ya kifahari na mengine ya kutanulia.
Alieleza kwa kirefu jinsi dawa hizo zinavyomezwa na kusafirishwa na kukanusha madai kuwa yanaingizwa tumboni kupitia njia ya haja kubwa. Alisema yanamezwa kama vidonge vingine baada ya kufungwa ndani ya vifuko ya nailoni, kisha kuzungushiwa gundi ya karatasi ya nailoni, kuzongwa na vipande vya glovu nyepesi ambazo hufungwa kikamilifu na kuchomwa kwa moto kama pipi kifua ili kuvidhibiti visifunguke na dawa kuyeyuka tumboni. “Kete zinazomezwa zina ukubwa wa kidole gumba cha mtu mzima na hutofautiana kwa uzito, zipo zenye gramu 10 na ndogo zina gramu tano.
Ukiwa mzoefu unaweza kumeza hata 100 na kubeba pipi zenye uzito wa kilo moja. ”
Mchungaji huyo ambaye sasa anasema anachohitaji ni kuwaeleza watu kuwa Mungu hapendi biashara ya madawa na kutangaza wokovu, na kusisitiza kuwa aliyemuondoa kwenye biashara hiyo ni Yesu Kristo. *Mahojiano kamili kuhusu jinsi Mwakisambwe alivyoanza kuuza mihadarati, nchi alizotembelea, majina aliyotumia, familia yake, mtandao wa nje na ndani alioshirikiana nao na jinsi alivyokutana na Yesu akamuokoa, zitachapishwa kesho kwenye Safu ya NIPASHE Jumapili ya Anayemulikwa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni