Kuna Nguvu Katika Mawazo Yetu – Sehemu ya 1
Je, mawazo yana athari au mchango katika
uhusiano wetu na Mungu? Je, yanaweza kutumika kuboresha uhusiano huo?
Kila mmoja wetu
huwa anawaza mambo mbalimbali kila wakati, maadamu tuko macho. Wakati mwingine
huwa tunawaza kwa kuamua na wakati mwingine huonekana kana kwamba mawazo fulani
yanavamia tu akili zetu; na kila tukijitahidi kuyaondoa inakuwa ni vigumu.
Kuwaza ni kipawa
cha muhimu sana
alichotupatia Mungu kwa ajili ya kutuwezesha kukua katika kumjua Yeye na
kuimarisha wokovu wetu na pia kuishi kwa mafanikio katika ulimwengu huu.
Akili ya
mwanadamu imeumbwa kwa namna ambayo haiwezi kutulia bila kuwaza. Maadamu uko
macho, akili huwaza muda wote – mara jambo hili, mara jambo lile.
Aina za
mawazo
Kuna aina kuu
mbili za mawazo, yaani mawazo yanayokuja yenyewe akilini (unconscious thoughts) na mawazo
tunayoamua wenyewe kuyawaza (conscious
thoughts), yaani kwa utashi wetu.
Mawazo
yanayokuja yenyewe
Mawazo ya aina
hii ndiyo mengi zaidi kwa watu walio wengi. Tena, mengi ya mawazo haya ni yale
yanayohusu matatizo, mapungufu au vikwazo mbalimbali. Hivyo, haya husababisha
mtu akose amani na furaha.
Mawazo ya
kuamua
Mawazo ambayo mtu
huwa unayawaza kwa kukusudia ni mawazo ambayo unayachagua. Kwa mfano,
unapokutana na jambo gumu ambalo unatakiwa ulitolee uamuzi, mara nyingi
utasema, “Hebu nipe muda nifikirie.” Hapa, unaenda kukaa mahali penye utulivu
na unaanza kulichambua wazo hilo
hadi unafikia uamuzi fulani.
Kutafakari
Kutafakari ni
kitendo cha kutumia akili zetu kuwaza kwa undani kuhusu jambo au wazo moja tu
bila kuchanganya na mawazo mengine.
Ni kitendo cha
kuchokoachokoa wazo au jambo hilo
hadi unatambua mambo yaliyojificha ndani yake. Kutafakari ni jambo
linalofanyikia moyoni wakati kunapokuwa na hali ya utulivu kabisa.
Kutafakari jambo
ni kama kutafuna kipande cha nyama taratibu. Kwanza unaweka mdomoni kipande kikubwa. Kisha unatafuna,
na kutafuna, na kutafuna hadi kinasagika na kuwa vipande vidogo vidogo.
Unapotafakari,
hali kadhalika unaanza na wazo moja kubwa. Kwa mfano, “Kwa kupigwa kwake sisi
tumepona.” (1Petro 2:24).
Ukishaingiza
akilini wazo hili, unatulia na kufunga mambo mengine yasiyohusiana nalo. Kisha,
unaelekeza akili yako yote kwenye wazo hilo.
Hatimaye unaanza kulivunjavunja. Kwa mfano:
- Anaposema ‘sisi tumepona’ ina maana na mimi ni mmojawapo.
- Anaposema ‘tumepona’ na wala si ‘tutapona’ ina maana tumepona sasa.
- ‘Tumepona’ pia ina maana ni kila ugonjwa na kila tatizo – maana hajataja ugonjwa au tatizo fulani maalum.
- Kwa hiyo, ugonjwa huu unaonisumbua au tatizo hili nililo nalo si langu.
- Ni Mungu kasema nimepona!
- Kile ambacho macho yangu yanaona, yaani ugonjwa au tatizo, ni uongo tu wa shetani.
- Kile anachosema Mungu, kuwa nimepona, ndiyo kweli halisi! Kwa vile shetani ni mwongo na Yesu ni mkweli, basi ninashikilia kweli ya Yesu.
Uhusiano
wa mawazo na maisha yetu
Maisha ni picha ya
mawazo
Ukiyaangalia
maisha ya mtu na yeye mwenyewe alivyo, unaweza kwa kiasi fulani kufahamu aina ya mawazo - si mawazo yenyewe -
ambayo huwa anawaza.
Biblia inasema,
“Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; bali moyo uliopondeka huikausha mifupa.” (Mithali 17:22). Moyo ukiwa umechangamka,
changamko lake hilo hudhihirika kwa nje.
Vivyo hivyo, moyo
ukiwa umenyong’onyea, nao hudhihirishwa na dalili zinazoonekana kwa nje. Mawazo
unayowaza ni nguvu halisi kabisa!
Vile ulivyo sasa,
ndivyo na mawazo yako yalivyo. Huwezi kuwa na maisha yanayovuka kiwango cha
mawazo yako. Aina ya mawazo uliyo nayo, ndiyo iliyokufikisha hapo ulipo. Je, ni
mawazo ya kuweza au kushindwa? Ni mawazo ya ujasiri au hofu? Ni mawazo ya
kupona au kuendelea kuumwa? Ni mawazo ya kupata au kukosa?
Si kwamba hali
uliyonayo ndiyo iliyosababisha mawazo uliyo nayo. Hapana! Bali, mawazo ambayo
umekuwa nayo, hata kama ni bila kujua, ndiyo
yaliyozaa hali uliyo nayo sasa. Ni mambo ambayo umetoka nayo mbali.
Uliyonayo sasa ni
matunda ya mapando uliyopanda kule nyuma mawazoni mwako. “Maana aonavyo nafsini
mwake ndivyo alivyo.” (Mithali 23:7).
Vivyo hivyo, yale
unayopanda sasa, utavuna matunda yake muda ujao. Kwa maana imeandikwa,
“Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho
atakachovuna.” (Wagalatia 6:7).
Mtu anaweza
akasema, “Akili yangu haijatulia kabisa. Sina amani moyoni. Nadhani ni kwa
sababu ya tatizo A au B.” Ili maisha yetu
yabadilike, wajibu wetu hasa si kuomba hali inayokuzunguka ibadilike ili mioyo
yetu itulie, bali ni kubadili mawazo yetu ili yaendane na Neno la Mungu.
Mabadiliko hayo ndani yetu ndiyo
yatasababisha
hali iliyo nje isalimu amri na kubadilika.
Kwa mfano, hali
inayokukabili yaweza kuwa ni mtoto mtukutu anayekusumbua hadi moyo wako unakosa
raha. Ukishakosa raha moyoni, utaanza kusema, “Jamani, mimi mtoto huyu
amenichosha. Mungu naomba mfanye abadilike ili moyo wangu utulie.” Kwa jinsi
hiyo huwezi kufanikisha lolote maana, katika hali halisi, ndani yako bado una
mtizamo wa kwamba, jambo hili ni gumu sana.
Ulichofanya hapo ni kunung’unika tu.
Lakini ukiamua
kubadili mawazo yako ukasema, “Naamini mwanangu atabadilika. Ni lazima
abadilike kwa Jina la Yesu! Asante
Yesu.” Unasema hivi huku mwanao bado ni msumbufu vilevile. Hapa umeelekeza
mawazo yako kwenye mtizamo wa ‘inawezekana’ kwa kumwamini Mungu. Kwa kubadilika
ndani yako
namna hii, ni
lazima utasababisha mabadiliko nje yako, yaani kwa mwanao. Lazima!
Je, wewe
unajionaje mwenyewe? Unaweza kujiweka katika kundi la watu wanaojiona wanaweza
au wanaojiona hawawezi? Je, unajiona umebarikiwa au unajiona una bahati mbaya?
Kuna uhusiano wa
moja kwa moja kati ya maisha ya mtu yalivyo na vile anavyojiona mwenyewe, yaani
anavyowaza moyoni mwake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni