Ijumaa, 1 Novemba 2013

LAANA YA KULA DAMU AU KUMWAGA DAMU

LAANA YA KULA DAMU AU KUMWAGA DAMU

Mchungaji Frank Andrew (Resident Pastor)

                                                         Na Mch. Frank Andrew (RP)

Ukisoma biblia utagundua kuwa Mungu ndiye wa kwanza kumwaga damu kwa sababu maalumu, ukisoma kuanzia Mwanzo sura ya tatu na kuendelea utaona baada ya uasi wa Adamu na Hawa, Mungu alichinja kondoo na kuwavika ili kuficha uchi wao. Kwa tafsiri damu ile ambayo Mungu aliimwaga kwa kumchinja kondoo ni kwaajili ya kufunika dhambi. Kimsingi kufunika dhambi ni tofauti na kuondoa dhambi hivyo inatofautishwa na damu ya Yesu kwa vile damu ya Yesu huondoa dhambi, kutokea hapo tunajifunza kuwa damu ya wanyama yaweza kutumika kufunika dhambi na ndivyo ilivyokuwa ikitumika katika agano la kale.

Kwa namna hiyo, damu ilikuwa kama kipatanishi kati ya mwanadamu na Mungu. Kwa wakati ule, damu hiyo ilitumika kama alama ya kuonyesha ukombozi wa mwanadamu utakaokuja kwa njia ya Yesu Kristo. Hivyo damu ilikuwa na thamani ya uhai wa mtu, kwasababu ilifunika dhambi (ambayo hukumu yake ni kifo) kwasababu hii Mungu akasema watu wasile mnyama pamoja na damu kwasababu kwenye damu kuna uhai. Kwasababu hiyo leo tunakwenda kuangalia kuhusu laana ipatikanayo kwa kumwaga au kula damu.

Laana ya kula damu:
Mwanzo 9:4 "Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile.
5 Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu."
Mungu anasema hakika; kumbe tangu mwanzo Mungu alikuwa kinyume na wale wanaokula nyama pamoja na damu. Kwasababu damu ya mnyama ina uhai ndani yake, hili ni chukizo mbele za Bwana na kwasababu hii watu wengi wameishi katika laana kubwa kwasababu ya kula nyama pamoja na damu yake.

Ndio maana watu wengi wanaofanya haya huishia kwenye matatizo ya kunywa damu yanayosababishwa na ule uhai uliyo ndani yake, na hivyo kumfanya Mungu ahitaji damu zao sawasawa na neno lake. Ukifuatilia katika makabila mengine, hula damu kama chakula, na hii inakuwa laana katika maisha yao na kwasababu hii watu huishia kufa vifo vya ajabu au kupata matatizo ya kuishiwa damu. Watu kama hawa hujikuta kwenye matukio ya kumwaga damu mara kwa mara kwasababu ya laana inayotokana na kula au kunywa damu, na kama mtu hana maarifa huisi kuwa ni wachawi wamemloga tu, lakini kumbe mlango wa kwanza uliomfanya shetani apate nafasi katika maisha yako ni ile laana ya kunywa damu.
NINAAMURU KAMA UMEWAHI KUNYWA DAMU, LAANA HIYO IVUNJIKE KWENYE MAISHA YAKO KATIKA JINA LA YESU.

Kumwaga damu ya Mwanadamu:
Katika kitabu cha Mwanzo 9:6 Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu.
Sababu nyingine ya damu kutakiwa ni kwa kumwaga damu ya mtu mwingine, hii ni laana inayompata mtu ikitokea amemuua mtu mwingine ama kichawi au kwa njia ya kawaida. Ndio maana koo ambazo zinahistoria ya uchawi ama baba au bibi watu wake hufanana kwa vifo vya kumwaga damu. Familia kama hizo huishia katika ajali za magari, kuumia ilimradi tu umwage damu.

Laana hii pia hufuatilia koo za machifu ambazo kipindi kile walikuwa wanamzika chifu na mtu akiwa hai au mtoto; ile laana hufuatilia koo hizo na inaweza kuleta vifo vya aina hiyo. Mwanzo 4:10 Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.
11 Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;
12 utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.
13 Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.
14 Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

Amwagaye damu ya mwanadamu na damu yake mtu huyo itamwagwa na mwanadamu mwingine, laana hii yaweza kumfanya mtu akose kikao duniani yaani mtu hawezi kutulia mahali pamoja. Ndio maana waweza kumwona mtu anakataliwa na kila mtu kumbe ni kwasababu ya laana iliyotokana na damu iliyomwagika. Sio lazima awe mtu mwenyewe, bali inawezekana baba au mama ndio waliomwaga damu na kwasababu laana yaweza kupiliza katika vizazi ikakufikia. Ndio maana maandiko yanasema, Yeremia 50:6 "Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.
Laana ni mbaya kwasababu inakushambulia bila kujua."

Laana hii pia yaweza kuja kwa kutoa mimba (abortion) yaani kuua kiumbe kabla hakijazaliwa na kwasababu hiyo mtu anakuwa na laana, na hii laana ya kutoa mimba inafuatilia kuanzia mwenye mimba, mtoa nauli, mshauri, msindikizaji na daktari mtoaji mimba, wote wapo chini ya laana. Mwanzo 6: 9 "Na alipoifungua muhuri ya tano, nikaona chini ya madhabahu roho zao waliochinjwa kwa ajili ya neno la Mungu, na kwa ajili ya ushuhuda waliokuwa nao.
10 Wakalia kwa sauti kuu, wakisema, Ee Mola, Mtakatifu, Mwenye kweli, hata lini kutokuhukumu, wala kuipatia haki damu yetu kwa hao wakaao juu ya nchi?"
Damu iliyomwagwa inamlilia Mungu juu ya malipizi yake. Ni muhimu kuvunja laana zote katika Jina la yesu ili kuwa huru kwelikweli.

Pamoja na haya yote ni muhimu kujua kuwa laana hizi haziwezi ondolewa kwa kujiua au kukata tamaa lakini damu ya Yesu Kristo, mtu asiye na dhambi yaweza kukutakasa kutoka katika uchungu na laana zote. Laana zote ziliondolewa zote pale msalabani, mpokee Yesu ili uweze kusimama kinyume na laana zote za maisha yako. Baada ya kumpokea Yesu hatua inayofuata ni kujiweka huru kutoka katika laana zote ambazo zinatesa maisha yako.MUNGU akubariki

source:    Ufufuo na Uzima GCTC

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni