Jumamosi, 9 Novemba 2013

Je, Sabato Ni Siku Katika Juma?



Je, Sabato Ni Siku Katika Juma?



Sabato ilianzia wakati wa uumbaji ambapo baada ya siku sita za uumbaji, Mungu alipumzika siku ya saba. 

Imeandikwa: Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya, akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. (Mwa. 2:2-3).

Hatimaye ulifika wakati ambapo Mungu aliwatoa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri; ndipo aliwapa amri juu ya sabato. 


Imeandikwa: Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote ... (Kut. 20:8-9).

MAANA YA NENO ‘SABATO’

Sabato ni neno linalotokana na neno la Kiebrania ‘shabbat’ ambalo lina maana ya kusimamisha, kukomesha, kuacha, au kupumzika. Hii ina maana ya kusimamisha jambo fulani, kulifanya likome kuendelea, au kuacha kutenda kitu fulani.

Kwa hiyo, kwa upande wa maisha ya kila siku ilimaanisha kwamba ikifika siku ya sabato, kazi zote zikome; watu wasimame au waache kufanya kazi zao ambazo walikuwa wanazifanya kwa siku sita zilizotangulia. Ilimaanisha kuwa watu wapumzike.

NAMNA SABATO ILIVYOTUNZWA

Katika kutekeleza amri ya Mungu, yalikuwapo mambo mengi yaliyoambatana na utunzaji wa sabato, ambayo kwa ujumla wake yamebebwa na maneno “usifanye kazi yoyote” (Kut. 20:10) , au kwa namna nyingine “pumzika” au “starehe”. 

Imeandikwa: Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa takatifu kwa BWANA. (Kut. 31:15).

Sasa, mambo ambayo yaliambatana na huo utunzaji wa sabato, yaani ambayo yalizuiwa kufanywa, ni pamoja na haya yafuatayo:

Kufanya biashara

Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki, na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo Yerusalemu. Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato? (Neh. 13:16-17).

Kubeba mizigo

Bwana asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue mzigo wowote siku ya sabato. (Yer. 17:21). 

Ndiyo maana Bwana Yesu alipomponya mtu aliyekuwa hawezi kwa muda wa miaka thelathini na nane na kumwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. (Yoh. 5:8), Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwabia, Leo ni siku ya sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. (Yoh. 5:10).



Kukusanya kuni

Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwapo jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya sabato ... wakamleta kwa Musa ... BWANA  akamwambia Musa, Mtu huyo lazima atauawa. (Hes. 15:32-35).

Kuwasha moto/kupika

Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya Sabato. Hii ina maana kwamba haikuruhusiwa kupika vyakula siku ya sabato. (Kut. 35:3).

Kutembea mwendo mrefu

Kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote asiondoke mahali pake kwa siku ya saba. (Kut. 16:29).

Kulikuwa na kiasi kinachoruhusiwa cha mtu kutembea inapofika siku ya sabato (Mdo 1:12). Ilikuwa ni makosa kwa mtu kwenda mwendo unaozidi kiasi hicho.

ADHABU YA KUVUNJA SABATO

Mtu ambaye aliasi sheria ya sabato, adhabu yake ilikuwa ni kuuawa.
Maandiko yanasema: Kila mtu atakayefanya kazi yoyote siku ya sabato, hakika yake atauawa. (Kut. 31:15b).

VIPINDI VITATU VYA MAISHA YA MWANADAMU

Mungu ameweka safari yetu yote ya kiroho katika nyakati au vipindi vikuu vitatu. Tunaweza kuviita vipindi hivyo kuwa ni: kipindi cha mfano, kipindi cha uhalisia wa kwanza, na kipindi cha utimilifu wa yote.

KIPINDI CHA MFANO 

Hiki ni kipindi ambacho kilihusu utimizaji wa maagizo ya Mungu kimwili. Kilikuwa ni kipindi cha maisha ya wana wa Israeli katika nyakati za Biblia.
Maandiko yanasema juu ya kipindi hiki kwamba: Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Kor. 10:11).

Hii inamaanisha kwamba, maisha ya wana wa Israeli waliyoishi kimwili yalikuwa ni mfano wa mambo ya rohoni ambayo Mungu aliyakusudia kwa ajili yetu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Lakini kabla hajayadhihirisha kwa ulimwengu wote makusudi yake hayo ya kiroho, aliyaonyesha kwanza kimwili kwa kutumia maisha halisi ya watu wachache, yaani Waisraeli. 

Pia imeandikwa: Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zilezile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. (Ebr. 20:1).

Maisha ya wana wa Israeli yaliongozwa na torati ambayo walifundishwa na Mungu kupitia Musa. Torati hiyo haikuwa jambo lenyewe halisi, bali ilikuwa ni taswira au picha ya kile ambacho ndicho hasa alikusudia Mungu, si tu kwa Israeli, bali kwa ulimwengu wote.

Katika kipindi hiki, watu walihesabiwa haki kwa kutenda matendo ya sheria (torati) kimwili kabisa. Ndiyo maana Mungu akasema: ... mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi BWANA. (Law. 18:5).

Pia imeandikwa: Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo. (Gal. 3:12).

Maana ya maneno haya ni kuwa, ukitaka uishi unaweza kufanya hivyo kwa kuitimiza torati YOTE! Ukiishi kwa torati halafu ukaivunja, basi utakufa. Na wakati huo watu walikufa kimwili kabisa, kwa mfano kwa kupigwa kwa mawe.

Tumesema kwamba torati ilikuwa ni sheria ya Mungu ambayo ilitekelezwa kimwili. Kabla hatujaangalia jinsi ambavyo sabato nayo ilikuwa ni ya kimwili, ifuatayo ni mifano mbalimbali ya jinsi Waisraeli walivyotekeleza torati kimwili:

Msamaha wa dhambi

Mtu alipotenda dhambi, ili aweze kusamehewa dhambi zake, ilimbidi aende kwa kuhani na mnyama halisi. 

… nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho juu ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa ajili ya nafsi. (Law.17:11).

Mavazi

Imeandikwa: ... wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja. (Law. 19:19b). Usivae nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja. (Kumb. 22:11). Hii ilikuwa ni amri iliyohusu nguo halisi kabisa zinazovaliwa mwilini.

Kutembelewa na Bwana

Bwana alipotaka kuwatembelea watu wake, watu walifua nguo halisi kabisa walizovaa mwilini. Imeandikwa: Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao, wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. (Kut. 19:10-11).

Vyakula

Haikuruhusiwa kula baadhi ya vyakula kwa kuwa vilitajwa kuwa ni najisi. Imeandikwa: Usile kitu chochote kichukizacho. ... msile katika wale wenye kucheua, na hao waliopasuliwa ukwato; ngamia, na sungura, na kwang’a, kwa kuwa hucheua, lakini hawakupasuliwa kwato, ni najisi kwenu; na nguruwe, kwa kuwa amepasuliwa ukwato lakini hacheui, huyu ni najisi kwenu, msile nyama zao, wala mizoga yao msiiguse. (Kumb. 14:3,7,8).

Kutoka utumwani

Waisraeli walitoka utumwani kwenye nchi Misri ya kimwili yenye Farao wa kimwili, wakapita kwenye jangwa la kimwili, na hatimaye wakaelekea kwenye Kanaani ya kimwili. 

Imeandikwa: Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, akawachunga kama kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, bali bahari iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, mlima alioununua kwa mkono wake wa kuume. Akawafukuza mataifa mbele yao, akawapimia urithi kwa kamba, na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao. (Zab. 78:52-55).

KIPINDI CHA UHALISIA WA KWANZA

Hiki ni kipindi cha kupokea ahadi za Mungu na kuishi kwa imani. Kile kilichokuwa mfano, kinakuwa ni kitu halisi. Hata hivyo, uhalisi huu si utimilifu wa kudumu kwa sababu kipindi hiki nacho kitabadilika na kuwa bora zaidi.
Hapa mambo yale ya Agano la Kale bado yanatendeka vilevile kama zamani, lakini si kimwili tena, bali ni kiroho. Kipindi hiki kilianza na ujio wa Bwana Yesu hapa duniani, na kinaendelea hadi sasa.

Hebu tuangalie jinsi mambo tuliyoongelea hapo juu yanavyotendeka katika kipindi hiki:

Msamaha wa dhambi

Bado sheria ni ileile kabisa. Hata leo bado tunatoa kafara ya damu ili kusamehewa dhambi zetu. Tofauti tu ni kwamba hatutoi tena wanyama halisi kama zamani. Wanyama waliotolewa kafara katika Agano la Kale walikuwa ni kivuli au taswira ya kafara timilifu, yaani Mwana-Kondoo wa Mungu, Yesu Kristo. 

Octagon: 18



Yohana alipomwona Yesu alisema: Tazama Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu. (Yoh. 1:29). Kama ambavyo zamani wanyama waliuawa kwa niaba ya mtenda dhambi, yaani walibebeshwa dhambi zake, ndivyo ambavyo Mwana-Kondoo wa Mungu alivyobebeshwa dhambi ya ulimwengu wote, kisha akatolewa kafara kwa niaba ya ulimwengu wote.

Ndiyo maana maandiko yanamwongelea Bwana Yesu kuwa ni: Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake. (Ufu. 1:5).

Mavazi

Hata leo sheria ya kutovaa mavazi yaliyochanganya rangi bado iko palepale.
Pia imeandikwa: Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki ... (Isa. 61:10).

Mavazi ni ishara ya wokovu. Wokovu ni mmoja tu. Hauwezi kupatikana kwa njia nyingine tofauti na iliyowekwa na Mungu. 

Maandiko yanasema: Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote,  kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. (Mdo. 4:12), yaani ni jina la Yesu pekee. Kutafuta wokovu kwa kutumia dini, imani au jambo jingine lolote nje ya Yesu ni kujivika mavazi ya rangi nyingi. Vazi la wokovu ni la rangi moja tu; nyeupe!

Kutembelewa na Bwana

Bwana alipokuwa anamuandaa Paulo kwa utumishi, Anania anamwambia Paulo: Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake. (Mdo. 22:16).

Halikuwa tena suala la kumwambia Paulo asimame akafue nguo alizovaa mwilini mwake.

Biblia pia inasema juu yetu kwamba: Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu. (1 Kor. 6:11).

Hii inaonyesha kwamba suala la kuosha au kufua bado liko palepale. Isipokuwa sasa kinachooshwa si nguo zilizoko mwilini bali ni uchafu uliomo moyoni, yaani dhambi. Na kinachoosha si tena maji ya kimwili, bali ni damu ya Yesu na Neno lake.

Vyakula 

Chakula kazi yake ni kutia uzima kwenye mwili. Kama ilivyokuwa katika Agano la Kale, hata sasa kuna vyakula vilivyo safi na vyakula visivyo safi, yaani ambavyo ni najisi. 

Bwana anasema wazi kwamba: Mimi ndimi chakula chenye uzima kishukacho toka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. (Yoh. 6:51).

Tunafahamu kwamba Yesu ni Neno la Mungu (Yoh. 1:1). Kwa hiyo, kula chakula najisi ni kuingiza moyoni maneno yasiyo ya Mungu kiasi kwamba nafsi inajaa takataka na uchafu; mawazo mabaya, hisia mbaya, n.k.

Ndiyo maana Bwana akaongea wazi kwamba: Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. (Mt. 15:11).

Uovu wa mtu haufiki rohoni kupitia tumboni kwa njia ya chakula. Pia roho ya mtu haili wali au nyama au ugali, bali hula Neno. Biblia inasema: Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. (Yoh. 6:63).

Yakiingia maneno ya Kristo moyoni, unapata uzima na afya ya kiroho, lakini yakiingia maneno mengine, hicho ni chakula najisi. 

Lakini kuhusu chakula cha kimwili, Biblia inasema: Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu, wala tukila, hatuongezewi kitu. (1 Kor. 8:8).

Kutolewa utumwani

Waisraeli walitolewa katika nchi ya utumwa kwa mkono hodari  wa Mungu aliye hai. Haikuwa ni kwa uwezo wao wenyewe, maana wangekuwa na uwezo wasingekaa utumwani kwa miaka mia nne na thelathini. 

Bwana anamwambia Musa: Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa, nami nitawatwaeni kuwa watu wangu. (Kut. 6: 6-7). Na hivyo ndivyo Bwana alivyofanya.

Hata leo hali iko vilevile. Hakuna mtu anayetaka kuishi sawasawa na sheria ya Mungu. Kila mtu anavutwa na hali ya dhambi iliyoko ndani yetu. Lakini unafika wakati ambapo mtu anachoka, na kutokea ndani ya moyo wake anaanza kumlilia Mungu. Naye Bwana anamimina neema ya wokovu juu yake.
Maandiko yanasema: Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. (Efe. 2:4-5). 

Hakuna mtu anayeweza kujisifia kuokoka. Ni neema ya Mungu tu. Bwana anasema: Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa. (Tito 2:11).  Ukiwa dhambini kutoka humo si jambo rahisi, ni kifungo kigumu mno!

Kuokoka, yaani kumwamini Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako binafsi ndio kutolewa kwenye utumwa wa Farao mtesaji, yaani ibilisi. 

KIPINDI CHA UTIMILIFU WA YOTE

Hiki ni kipindi ambacho tutakuwa katika miili ya utukufu, yaani ni baada ya maisha haya ya duniani. Tutakuwa katika Yerusalemu mpya na hatutahitaji tena imani maana kile tulichokuwa tukikiamini kitaonekana wazi na tutakiishi jinsi kilivyo milele na milele! 

Biblia inasema kwamba: Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. (1 Kor. 13:12).

Hebu tuangalie baadhi ya vipengele ambavyo tumekuwa tunaviongelea kwenye vipindi viwili vya mwanzo hapo juu jinsi ambavyo vitakuwa katika kipindi cha utimilifu wa mambo yote.

Msamaha wa dhambi

Katika kipindi cha kwanza mtu aliyetenda dhambi alitoa mnyama wa kafara ambaye alikufa kwa niaba yake. Katika kipindi cha pili, tunatoa damu ya Yesu kwa imani. Hata hivyo, katika kipindi cha ukamilifu, wale walio mbinguni hawatakuwa tena na kazi ya kuomba msamaha maana kule hawatendi tena dhambi. 

Maandiko yanasema kuhusu Yerusalemu mpya: Na ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:27).

Tuwapo hapa duniani tunao unyonge wa dhambi ndiyo maana Bwana anasema:  mtakatifu na azidi kutakaswa. (Ufu. 22:11). Wewe ni mtakatifu tayari kwa njia ya wokovu ulio katika Kristo Yesu. Lakini, kutokana na kwamba bado uko duniani, utafanya kosa hili na lile. Ndiyo maana Bwana anasema ‘mtakatifu na azidi’ kujitakasa.

Mavazi

Katika kipindi cha kwanza haikuruhusiwa kuvaa mavazi halisi yenye rangi tofautitofauti. 

Katika  kipindi cha pili, mavazi ni wokovu. Hivyo, kuwa na vazi la aina moja ni kusimama na wokovu halisi wa Yesu Kristo bila kuuchanganya na mambo ya kidunia. 

Hata hivyo, katika kipindi cha utimilifu wa yote, mbinguni kuna mavazi halisi ya haki yaliyo ya milele, ambayo yatakuwa safi siku zote; milele na milele.
Imeandikwa: Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe ... (Ufu. 7:9). Haya ni mavazi ambayo yameoshwa kwa damu ya Mwana-Kondoo wa Mungu.

Kutembelewa na Bwana

Katika kipindi cha kwanza, watu walifua mavazi yao halisi ya mwilini ndipo Bwana alikuja kusema nao. Mavazi hayo yalifuliwa kwa maji halisi.
Katika kipindi cha pili, kinachooshwa si mavazi halisi ya mwilini, bali ni dhambi katika mioyo yetu. Dhambi hizo zinaoshwa kwa njia ya damu ya Yesu Kristo.

Katika kipindi cha tatu, yaani cha utimilifu kwa yote, si tu kwamba hakutakuwa tena na haja ya kuoshwa (maana wote watakuwa watakatifu milele), lakini pia hakutakuwa na kusema kuwa kuna kutembelewa na Bwana, maana watakatifu watakuwa naye siku zote. 

Imeandikwa: Nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.  wala hapatakuwa na usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu huwatia nuru, nao watatawala milele na milele. (Ufu. 22:4-5).

VIPINDI VITATU VYA SABATO

Baada ya kuangalia vipindi vikuu vitatu vya uumbaji kuhusiana na mwanadamu kwa kirefu namna hiyo, hebu tuangalie sasa kama sabato nayo inapita katika vipindi hivyo vitatu.

Kipindi cha mfano

Kama ilivyo kwa mambo mengine, sabato nayo ilianza na kipindi cha mfano. Hiki kilikuwa ni kipindi cha Agano la Kale ambacho kilitekelezwa kwa kupitia watu kupumzika kimwili kabisa.

Hii haikuwa ni hali ambayo Mungu alipanga iendelee hivyo hivyo siku zote, bali alikusudia tulione kusudi lake lililo kuu zaidi kupitia kipindi hicho cha mfano. 

Kupitia sabato Mungu alikuwa anasema nasi juu ya kitu kingine bora zaidi. Si makusudi yake mawazo yetu yaishie tu kwenye kupumzika kimwili, kujizuia kazi za kimwili, n.k. Ndiyo maana anasema: Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. (Kol. 2:16-17).

Kipindi cha uhalisia wa kwanza

Hiki ni kipindi ambacho ni cha kiimani zaidi. Kimsingi hiki ni kipindi ambacho kinaendelea hadi sasa. Huu ni wakati wa kupumzika kazi za mwili za uovu, yaani kuacha dhambi na kuishi kwa kumtegemea Kristo. Ni maisha ya imani.
Imeandikwa: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28), yaani, nitawapa ‘sabato’. Pia ndiyo maana ya andiko lisemalo: Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato. (Mt. 12:8). Sabato iko kwake, si kwenye siku.

Ni maisha ya kujiachia mikononi mwa Mungu ambaye yeye ndiye anayeshughulikia kila kitu katika maisha yetu. Kazi yetu ni kuamini tu kuwa atafanya; naye hakika anafanya. Hilo ndilo pumziko! Hiyo ndiyo raha! Hiyo ndiyo starehe! Hiyo ndiyo sabato!

Kipindi cha utimilifu wa yote

Hiki ni kipindi cha maisha ya mbinguni. Huo utakuwa ni utimilifu wa yote kwa sababu, mara tutakapoingia humo, tutakuwa tukitekeleza sabato halisi milele na milele.

SABATO SI SIKU

Upo ushahidi wa kutosha katika Biblia unaoonyesha kwamba sabato si siku katika juma. Bwana anapoongelea kuhusu safari ya wana wa Israeli anasema:
Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, nikasema, Siku zote ni watu waliopotoka mioyo hawa ... hawataingia rahani mwangu. (Ebr. 3:10-11).

Pia imeandikwa: Maana ameinena siku ya saba mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu. (Ebr. 4:4-5).

Katika maandiko haya Mungu anasema kwamba, kutokana na kukasirishwa na uasi wa wana wa Israeli kule jangwani, alimua kwamba hawataingia kwenye raha aliyokuwa amewaandalia. Neno rahani hapa, au kwa Kiingereza rest, ndilo hilohilo sabato. Ndiyo maana hapo juu katika Ebr. 4:4-5, anahusisha siku ya saba na kuingia rahani.

Lakini hebu tujiulize maswali yafuatayo ili tuweze kupiga hatua zaidi.
  • Je, Israeli walipokuwa jangwani kwani hawakuwa wakitunza sabato kama siku? Jibu ni ndiyo, waliitunza. Biblia inasema: Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula  sehemu mara dufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA,Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA ... (Kut. 16:22-23).
  •  Kama basi waliitunza sabato, iweje tena Mungu aseme, ‘Hawataingia rahani mwangu’? Kama ingekuwa ni kumwuliza Mungu, mtu ungesema, “Bwana, unasemaje hawataingia rahani mwako wakati kila siku ya saba wanapumzika?” Hii ni ishara ya wazi kwamba sabato hasa si kupumzika au kutofanya kazi kimwili katika siku ya saba. Sabato ni jambo jingine tofauti na siku ya saba. Iko sabato halisi ambayo siku ya saba na kupumzika kwake vilikuwa ni kivuli chake tu.
  • Jambo jingine la kujiuliza ni kwamba, japo ni kweli kwamba wale ambao Mungu alisema hawataingia rahani mwake walifia wote jangwani, lakini walikuwapo wengine wengi walioingia, yaani watoto wao. Sasa je, hao walioingia waliipata hiyo raha (sabato)?

Mtu anaweza kujibu, Ndiyo, maana sote tunajua kuwa hata wakati alipokuja Bwana Yesu, alikuwa akifundisha mara nyingi kwenye masinagogi 'siku ya sabato'. Kwa hiyo, mtu anaweza kusema, ‘Ndiyo, waliingia kwenye raha au kwenye sabato.’

Lakini Mungu ambaye ndiye mwenye usemi wa mwisho juu ya mambo yake mwenyewe anasema:

Basi kwa kuwa neno hili limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake, msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha (yaani sabato), asingaliinena siku nyingine baadaye. Basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. (Ebr. 4:4-9).

Yaani, hawa watu licha ya kwamba kila mwisho wa wiki walikuwa wakipumzika, bado Mungu anasema ‘walikosa kuingia.’ Lakini cha kushangaza zaidi ni kwamba, kumbe hata siku yenyewe ilibadilishwa! Je, umeona hayo maneno ‘aweka tena siku fulani’? Pia hapo mwishoni nako anasema, ‘siku nyingine baadaye’!!

Hebu jiulize, inakuwaje siku nyingine wakati tumesema kwamba hadi Yesu anakuja watu hao walikuwa wakipumzika kila mwisho wa wiki?

Jibu ni wazi kwamba ‘siku nyingine’ hapa haimaanishi siku katika juma – maana hiyo haikuwahi kuachwa! Kwa hiyo, ni wazi kwamba, hii ni ‘siku ya sabato’ tofauti na ile iliyojulikana na kufuatwa tangu siku za Musa!

HOJA YA SABATO KUTOKA KINYWANI MWA MUNGU

Iko hoja kwamba sabato ni amri ya muhimu sana kwa sababu ilitoka moja kwa moja kinywani mwa Mungu tofauti na amri zingine ambazo zililetwa kupitia manabii au mitume.



Hoja hii haina uzito kwa sababu kuu mbili:

1.   Biblia kwa ujumla wake ni Neno la Mungu ambalo limetoka kinywani mwake lote. Na maandiko yako wazi kwamba: Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa, apate kutenda kila tendo jema. (2 Tim. 3:16-17).

Na kimsingi maandiko haya, ukisoma kwenye Biblia ya Kiingereza, hayasemi “Kila andiko lenye pumzi ya Mungu”. Badala yake yanasema: All Scripture is God-breathed (NIV); au All scripture is given by inspiration of God (KJV). Hii ina maana kwamba: Maandiko yote yametokana na pumzi ya Mungu.

Kwa hiyo, hakuna mantiki kusema kwamba andiko hili lina maana zaidi kuliko lile kwa kuwa hili alitamka Mungu mwenyewe. Yote yana nguvu ileile; yote yametoka kwa Mungu yuleyule.

2.   Sababu ya pili ni kuwa, Bwana Yesu alisema: Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma. (Mt. 10:40).

Maana yake ni kuwa Musa au nabii yeyote hakusema kwa niaba yake au kwa nafsi yake mwenyewe. Maneno waliyoyasema na kuyaandika hayakuwa yao.

Ukimpokea Musa au Paulo na maneno yake, unakuwa umempokea Kristo,  na hatimaye Mungu Baba mwenyewe.

Kwa hiyo, si sahihi kudhani kuwa maneno ya Musa au ya Paulo ni yake yeye, na kwamba yana uzito wa chini kuliko yale yaliyotoka kinywani mwa Mungu moja kwa moja kuhusiana na sabato. 

KWA NINI YESU ‘ALIVUNJA’ SABATO?

Hebu tuangalie mifano kadhaa hapa:

Mfano wa 1

Yesu alipomponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa muda wa miaka 38, alimwambia ‘jitwike godoro lako, uende.’ (Yoh. 58). Hii ilikuwa ni siku ya sabato.

Lakini tunaona kwamba Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwambia, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. (Yoh. 5:10). Bila shaka walisema hivi kwa kuwa walifahamu fika jinsi sabato inavyotakiwa kutunzwa.
Hii ni kusema kwamba, kwa kadiri ya kanuni za utekelezaji wa sabato, hili lilikuwa ni kosa. Sasa, swali ni kwamba, kwa nini Yesu alivunja sabato kwa kumruhusu yule mtu abebe godoro?

Mfano wa 2

Wayahudi walipomkasirikia Yesu kwa sababu ya kumruhusu yule mtu kubeba godoro siku ya sabato, Bwana Yesu aliwajibu kwamba: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. (Yoh. 5:17). Haya ni maneno ya ajabu sana. Wewe uliye Mungu ulituambia kwamba siku ya sabato tusifanye kazi bali tupumzike; tumemwona mtu anafanya kazi ya kubeba godoro, tumekuja kwako, lakini wewe si tu kwamba hukumkemea, bali unasema tena kwamba na wewe unafanya kazi hata sasa (siku ya sabato)!

Kama sabato hasa ni kuacha kufanya kazi, iweje tena Yesu atamke jambo ambalo ni wazi kabisa linavunja sheria aliyoiweka mwenyewe ya kutofanya kazi; yaani aseme kuwa hata sasa yeye anafanya kazi?

Mfano wa 3

Siku moja Yesu aliingia kwenye sinagogi ambamo mlikuwamo mwanamke mwenye pepo wa udhaifu. Yesu alimponya mama yule.

Hata hivyo, Biblia inasema: Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. (Lk. 13:14). 

Maneno haya ya mkuu wa sinagogi yanatuonyesha kwamba, jambo alilofanya Yesu lilikuwa ni kuvunja sabato. Swali ni lilelile, kwa nini Yesu alivunja sabato?

Tunafahamu kuwa maandiko yanasema kwamba kuvunja sabato ni dhambi, tena ambayo iliadhibiwa vikali sana. Na katika mifano hiyo hapo juu, tunaona kwamba Yesu alivunja sabato kwa kufanya mambo ambayo jamii nzima ilikuwa haiyafanyi siku ya sabato. Kwa harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba, Yesu alitenda dhambi.

Lakini wakati huohuo, maandiko yanasema kwamba, katika kuishi kwake kote hapa duniani, Bwana Yesu hakuwahi kutenda dhambi. (Ebr. 4:15).

Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, iweje uvunje sabato, jambo ambalo ni dhambi, halafu uhesabiwe kuwa hujatenda dhambi? Pili, iweje wewe ambaye ndiye ulisema watu wapumzike siku ya sabato, ndio uwe wa kufanya kinyume na agizo lako mwenyewe? (Maana Yesu ndiye Mungu aliyeagiza sheria ya sabato ifuatwe). Iweje hapa yeye ndiye awe wa kuivunja?

Hapa jibu ni moja tu. Sabato si siku katika juma! Kama sabato ingekuwa ni siku katika juma, Bwana Yesu angekuwa na hatia ya kuvunja sabato, maana ni wazi kuwa alitenda mambo ambayo ni kinyume na sabato kama siku!

Lakini kwa sababu sabato ina maana tofauti na siku, ndiyo maana aliruhusu mtu yule abebe godoro siku sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na uponyaji siku ya sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na wanafunzi kukwanyua masuke mashambani!

MAANA HALISI YA SABATO

Sabato ni kitu gani basi kama si siku katika juma? 

Maandiko yanasema: Basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye (yaani mwanadamu) aliyeingia katika raha yake (yaani raha ya Mungu) amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake. (Ebr. 4:10).

Aha! Kumbe sabato si kupumzisha damu na nyama katika siku mojawapo ya wiki; si kujizuia kukoka moto, kubeba mzigo au kusafiri mwendo mrefu kimwili!

Sabato ni kitendo au hali ya mwanadamu kuacha ‘kazi zake’ kama Mungu alivyoacha zake. Mungu ni mtakatifu, kwa hiyo kazi zake ni takatifu na kamilifu. Mwanadamu ni mpungufu, kwa hiyo kazi zake ni uasi, yaani dhambi. Hizo ndizo anazotakiwa kupumzika kwazo, yaani kuziacha na kumgeukia Mungu.

Ili kuweza kuingia rahani mwa Bwana, yaani kwenye sabato yake, Bwana akasema: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Matayo 11.28).

Pumziko au raha au sabato hiyo si kupumzisha damu na nyama katika siku fulani ya wiki, bali Bwana anasema: Nanyi mtapata raha (sabato) nafsini mwenu. (Mt. 11:29) – si kwenye miili yenu!

Na pale unapowezeshwa kuacha dhambi na ukamgeukia Bwana na kumfuata maishani mwako, ndipo raha au sabato hiyo inapokuwa ni kwa faida au kwa ajili yako, yaani sabato inakuwa ni kwa ajili ya mwanadamu. Lakini ukishikilia kutunza siku, hapo wewe ni kwa ajili ya siku (sabato) na wala si sabato kwa ajili yako.

Kwa hiyo, sabato si siku bali ni pumziko, raha na starehe ndani ya Kristo katika Roho Mtakatifu. Imeandikwa: Maana ufalme wa Mungu si kula wala kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. (Rum. 14:17).

HITIMISHO

Tumalizie kwa kujiuliza swali hili. Je, kuabudu siku ya sabato au jumamosi ni vibaya?

Yapo mambo mawili ya kutofautisha hapa. Kuna kushika siku kama siku tu; na kushika siku kama sehemu ya utekelezaji wa sheria.

Ukishika siku kama siku tu, unaweza kumwabudu Mungu katika siku yoyote upendayo maana siku zote ni sawa tu.

Lakini ukishika siku kama sheria, hutaweza kuabudu katika siku yoyote, maana sheria ina siku yake maalumu.

Kuabudu katika siku ya sabato (jumamosi) kama siku tu haina tatizo hata kidogo. Lakini kuabudu  katika siku hiyo kama sheria kunaweza kuwa na maswali. 

Tumeshaona kwa ushahidi mwingi kwamba, sabato ilikuwa ni kivuli au mfano au taswira ya kitu kingine.

Unapopita barabarani, utaona vibao vinavyotaja majina ya sehemu na umbali wake. Mathali unaweza kuona: ARUSHA, KM 350.

Kama wewe utaamua kushusha mizigo na kukaa kwenye kibao hicho kisa tu kimeandikwa Arusha ambako ndiko ulikokuwa unaenda, basi hapo liko tatizo.
Kibao ni ishara tu ya hiyo Arusha. Lakini iko Arusha yenyewe halisi. Kazi ya kibao ni kukuelekeza kwenye lengo au kusudi halisi la safari. Chenyewe si kusudi lenyewe.

Sabato iliwekwa ili iwe ni kibao cha kutuelekeza kwenye kusudi. Sasa wewe ukiing’ang’ania yenyewe ukaacha kusudi, basi hapo ndipo ilipo shida.Na kama utafika kwenye kusudi lenyewe, je, utang’ang’ania kibao cha nini tena?

Jambo la msingi ni kuwa, sabato au pumziko halisi ni kuwa ndani ya Yesu, yaani kuokoka. Ukishaingia ndani ya Yesu, haijalishi tena endapo utamwabudu siku ya kwanza, ya pili au ya mwisho ya juma.

Biblia inasema: Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine aona kuwa siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku, huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu; tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. (Rum. 14:5-6).

Tena imeandikwa: Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. (Kol. 2:16-17).

Vilevile imeandikwa: Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka. Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu. (Gal. 4:9-11). 

Je, umeokoka? Kama jibu ni ndiyo na unapenda kumwabudu Bwana wa sabato (pumziko) siku ya jumamosi, basi songa mbele katika hilo, maana siku kama siku haikuongezei wala kukupunguzia chochote.

Je, hujaokoka? Kama jibu ni ndiyo, nasikitika kusema kwamba kushika kwako siku hakutakusaidia, maana hapo hakuna tofauti na kung’ang’ania mfano au kibao na kuacha jambo lenyewe ambalo hasa ndilo lililolengwa na kibao au mfano huo.

Mtu akiwa mwizi, wizi wake hautoki kwa sababu ameabudu katika siku fulani ya juma. Na mtu mtakatifu, utakatifu wake hauji kutokana na kuabudu katika siku fulani. Utakatifu unatoka kwa Bwana wa sabato, Yesu Kristo mwenyewe.
Umeona mwenyewe hapo juu kwamba Mungu anaita ‘kushika siku’ kuwa ni ‘mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge!’

Achana na mambo ya kimwili maana wakati wake ulishapita! Bwana Yesu alisema wazi: Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. (Yoh. 4:23-24).
Si katika mwili!!

James John
Reactions: 

4 comments:

Asante sana mtumishi wa Mungu nimebarikiwa sana na neno hili.Mungu akutangulie uzidi kusonga mbele katika kuujenga mwili wa Kristo (Baba wa sabato)
Amina ndugu. Ubarikiwe na Bwana pia.
GODFRAY -TANZANIA,
Mungu akubariki mtumishi. kwa kweli somo hili linafungua kwa mapana na marefu. naamini linamtoa mtu katika mgando wa kiakili na kumfyatua kuelekea kwenye ukombozi halisi, kama Paulo mwenyewe alivyookolewa. Mungu akubariki.
Amen, Godfray. Bwana Yesu akubariki nawe pia. Ashukuriwe Bwana kama umeweza kupokea kitu kutoka kwake kupitia somo hili.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni