Saturday, September 7, 2013
VIFUNGO VYA MWILINI
Na Mch. Josephat
Gwajima
|
Utangulizi:
Mungu anawapenda sana
wanadamu na Biblia inasema wazi kuhusu hili katika kitabu cha Maombolezo
3:31; Ni raha yake kuona hatuna matatizo na tunaishi kwa amani. Mungu
hakumuumba mwanadamu ateseke bali alimuumba afanikiwe akiwa duniani na kuishi
kwa furaha.
Wakati huohuo, shetani kwa asili hapendi mtu aliyeumbwa na
Mungu afanikiwe na ndio maana katika Luka 3:16 inasema, “…ambaye shetani
amemfunga miaka kumi na minane…” (Matendo 10:38; 2Wathesalonike 2:18-19)
kwa maandiko hayo tunaweza kujua kuwa shetani anaweza kufunga, kuzuia, kupinga
na kushindana na mtu. Kwa asili shetani ni mshindani na furaha yake ni kuwatesa
wanadamu ambao wanapendwa na Mungu. Yeye hufanya hivi ili kuumiza moyo wa Mungu
kupitia wanadamu walioumbwa na Mungu.
SHETANI ANAWEZA KUMFUNGA MTU:
Kama tulivyoona kuwa shetani anapenda kuwatesa wanadamu na
ili kutimiza lengo lake
njia mojawapo anayotumia
ni kuwafunga watu. Na tunapotaja vifungo, tunakuwa tunazungumzia vifungo vya
aina kuu tatu, yaani, Vifungo vya mwilini, Vifungo vya rohoni na vifungo vya
nafsini kwasababu mtu ni roho inayokaa ndani ya nyumba iitwayo mwili. Katika
hatua hii ya kwanza tunaanza kuangalia kwa undani kuhusu vifungo vya mwilini:-
Mwili ni nini?
Hatuwezi kujua namna mwili unavyoweza kufungwa bila kujua
asili ya mwili wa binadamu. Tuanze kwa kuangalia andiko hili Mwanzo 2:7
“BWANA Mungu akamfanya mtu kutoka katika mavumbi ya ardhi…” kumbe asili ya
mwili wa mwanadamu ni mavumbi au udongo. Na ndio maana katika Isaya
64:8 Biblia inasema, “… sisi tu udongo nawe ni mfinyanzi wetu...” nabii
Isaya ambaye aliwahi kumuona Mungu lakini alijua ukweli huu kuwa mwili ni
mavumbi (Ayubu 7:21, 34:15). Kumbe pamoja na kuwa umevaa vizuri au
umeupamba mwili vizuri lakini asili yake ni udongo na katika ulimwengu wa roho
huonekana kuwa ni udongo kabisa. Kwa ufupi mwili wa mwanadamu ni udongo na mtu
anapokufa mwili huirudia nchi (Mhubiri 12:7) yaani mavumbi.
Ndio maana hata watu wanapooana ni miili ndio ambayo inakuwa
imeoana na si roho kwasababu mbinguni hakuna kuoa wala kuoana kule ni katika
roho. Kwa kujua kuwa mwili ni udongo basi namna ambayo unaweza kuutendea udongo
wa kawaida ndivyo vilevile waweza kuutendea mwili wa binadamu. Udongo wa
ardhini waweza kuoteshwa mimea na kuchimbwa, vilevile na mwili wa binadamu
waweza kufanyiwa hivyo.
TOFAUTI KATI YA MWILI NA UDONGO WA KAWAIDA:
Kuna mambo mawili makuu yanayosababisha mwili wa binadamu
uwe tofauti na udongo wa kawaida.
1. Mwili uliwahi kushikwa na mikono ya Mungu maana hakuna
kitu kilichowahi kushikwa na Mungu na kikabaki kama
kilivyo.
2. Ndani ya mwili wa mwanadamu kuna roho ambayo huuisha
mwili na kuupa uhai. Kwasababu hizo mwili wa mwanadamu hutofautina na udongo wa
kawaida.
MWILI WA MWANADAMU UNAWEZA KUPANDIWA VITU:
Biblia iko wazi kuwa Mungu wa mbinguni anaweza kupanda, (Mwanzo
2:8); kumbe Mungu ambaye ni roho (Yohana 4:24) anaweza kupanda
katika ardhi kabisa vivyo hivyo shetani naye ni roho naye ana uwezo wa kupanda
katika mwili ambao kwa asili ni udongo. Hapa ndipo lile andiko la “KILA PANDO
AMBALO BABA WA MBINGUNI HAKULIPANDA LITANG’OLEWA” linapoleta maana; Mapando
ambayo hayajapandwa na Baba wa mbinguni ni lazima yatakuwa yamepandwa na
shetani. Ndio maana ya mfano wa Yesu katika Mathayo 13:25 “lakini watu
walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.”
Huyo ambaye Yesu anamwita adui ni shetani mwenyewe. Kumbe unapolala au
kujisahau shetani huja na kupanda magugu, hili jambo linatendeka katika
ulimwengu wa roho. Ni muhimu kujua siri hii kwamba kama
vile udongo unavyopandwa vivyohivyo shetani naye anao uwezo wa kupanda juu ya
mwili wa mwanadamu.
Unaweza kumsikia mtu analalamika kuwa mwili unachoma lakini
kumbe katika ulimwengu wa roho mtu huyo amechomwa mkuki au kisu. Kufikia
hapa sasa twaweza kujua kwanini Mungu alikataza kupanda mbegu mbili za tofauti
katika shamba moja (Mambo ya Walawi 19:19). Mungu alisema hivi
akitufundisha kuwa mahali ambapo Mungu amepanda shetani hatakiwi kupanda mahali
pale. Mtu anaweza kuhisi vitu vinatembea mwilini kumbe amepandiwa
wanyama wanaotembea katika mwili wake.
PEPO ANAWEZA KUJIGEUZA NA KUWA CHOCHOTE:
Tulijifunza kuhusu sheria mbili za rohoni, hapo tuliona uwezo
wa pepo wachafu kujigeuza na kuwa kitu kingine yaani kuvaa sura mbali mbali ili
kutimiza kazi zao. Jambo hili twaweza kuliona katika (1Wafalme 22:19-23)
huyu pepo kwa asili hakuwa wa uongo lakini aliweza akaenda na akawa pepo wa
uongo. Yule pepo akaingia katika vinywa vya manabii wa Mfalme Ahabu na
kuwafanya wamtabirie uongo. Kwa maana hiyo tunaona uwezekano wa pepo mchafu
kujigeuza na kuwa kitu chochote ili kutimiza lengo alilokusudia.
Sasa twaweza jua kuwa mapando tuliyokuwa tunayazungumzia ni
pepo wachafu ambao hujigeuza na kuwa kile kitu na hivi ndivyo vinavyoitwa
“Vifungo vya mwilini”. Wakati mwingine pepo anaweza kujigeuza na kuwa kinywa
cha mtu, kama pepo wa katika (1wafalme
22:19-23) alivyofanya. Hivyo; unaweza kumuona mtu anatukana matusi ya ajabu
bila hata aibu, kumbe pepo kajigeuza na kuwa kinywa chake. Pepo anaweza kuwa
uso wa simba, unamkuta baba mwenye nyumba mkali kwa watoto na mkewe kumbe ni
uso wa simba. Kwahiyo; pepo wanaweza kujigeuza maumbo mbalimbali kama nyani, simba, paka hata bundi ili mradi kuharibu
hatma ya mtu. Mnamkuta dada aolewi kumbe uso wake umefunikwa kwa sura ya simba,
kila mwanaume anayetaka kumchumbia haoni sura nzuri bali anaona simba. Na ndio
maana kuna baadhi ya wadada watumia muda mwingi kujipodoa lakini bado hawapendezi
kwa kuwa uso sio wa kwake.
KUNG’OA KILA KILICHOPANDWA KATIKA MWILI WAKO:
Imeandikwa kila pando asilolipanda Baba wa mbinguni
litang’olewa, hivyo Mungu ametupa mamlaka ya kung’oa kila pando la kishetani
yaliyopandwa katika mwili. Miili yetu ni Hekalu la Roho Mtakatifu hivyo shetani
hatakiwi kugusa sehemu yoyote ya mwili wako.
Tumia mamlaka yako kung’oa kila pando ambalo shetani
amepanda katika maisha yako mapando ya magonjwa, homa zisizoisha, ukimwi,
mwasho wa mwili na matatizo mbalimbali. Jina la Yesu lina mamlaka yote dhidi ya
kazi zote za shetani katika maisha yako.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni