ROBO YA WATU DAR NI MISUKULE-12
ALINIPA bakuli akiniashiria nile lakini yeye akawa amesimama pale pale pembeni ya muuzaji akisubiri chombo hicho ili aondoke nacho. Nilikaa chini na kula kama nilivyoelekezwa. Muda wote wa kufanya hivyo, wateja walipungua na kutoingia dukani.Hapa nataka kusema jambo moja ambalo mtalielewa kwani ni la kawaida sana na hutokea kwenye jamii yetu. Mara nyingi, muda wa mchana, biashara hazichanganyi sana, uongo kweli?
Unaijua sababu SASA ENDELEA…
Naamini wengi mtajibu ni kweli. Sababu kubwa ni kwamba, biashara nyingi duniani zinaendeshwa kwa imani za kishirikina. Naweza kusema katika kila biashara mia moja, sitini na tano zinategemea ushirikina.
Ushirikina mwingi ni ule wa kuwepo kwa vitu, hasa misukule kwa ajili ya kuvuta wateja kwenye biashara hizo. Sasa kinachofanyika ni kwamba, hii misukule kazi yao kubwa ni kuita wateja kwa ishara kama niliyoisema.
Kazi hii hufanywa kwa muda mrefu kuanzia asubuhi hadi saa sita mchana ambapo hupumzika kula. Sasa katika kipindi hiki cha mlo, kwa sababu misukule huacha kuita, wateja nao hupunguza kasi ya kuingia kwenye maduka.
Hii hutokea hata kwenye maduka ya mtaani ambayo, wamiliki wake wanatumia misukule, ikifika wakati wa kula, utaona wateja ni wachache sana, hata wateja wenyewe kama wapo majumbani mwao hujisikia uvivu kutoka kwenda dukani.
Mara nyingi baada ya mlo hufuatiwa na mapumziko mafupi, lakini baada ya hapo shughuli uendelea. Ndiyo maana kuanzia saa nane na kuendelea biashara huchanganya tena kwa vile misukule mingi huwa imesimama ikiita wateja.
Sasa hili zoezi lina kitu kimoja cha ajabu, wamiliki ndiyo wanaojua kwamba yupo na msukule anayeitia wateja, lakini kuna wauzaji ambao huwa hawajui kama anauza akisaidiwa na misukule.
Ila kwa wale wauzaji ambao watataka kujua kuwa ndani ya duka analofanyia kazi kuna misukule atatakiwa kuangalia dalili hizi.
Mara nyingi akiwa ndani ya duka atakuwa anahisi kama kuna mtu anatembea, akishtuka anakuta hali ya utulivu.
Wakati mwingine akiwa amekaa atahisi damu zikimsisimka mwilini na nywele zikichachamaa. Hapo ina maana msukule umemfuata na kusimama nyuma yake kisha unamdhihaki kwa kumng’ong’a.
Akitoka kwenda chooni, akirudi na kuchunguza sana ndani ya duka ataona kuna mabadiliko. Lakini haya mabadiliko yanata kutumia akili sana kuyabaini. Mara nyingi mabadiliko haya ni mfano, gazeti liliwekwa likiwa limekunjwa ukurasa wa kwanza upo kwa ndani, lakini litakutwa ukurasa wa mwisho ndiyo uko kwa ndani wa kwanza upo nje.
Ndani ya duka ikipulizwa pafyumu ya aina yoyote, hata uchomwe udi, harufu yake haikai hata dakika tano. Wengi wamekuwa wakiamini pafyumu hiyo si nzuri lakini ukweli ni kwamba ni kwa sababu ya misukule. Wao humaliza harufu yoyote nzuri kwa uwepo wao tu.
Uzuri ni kwamba, misukule inayowekwa ndani ya maduka hushindwa kuzuia kuibwa kwa fedha, mfano mmiliki wa duka amemwajiri kijana kuuza, halafu kijana huyo akawa anaiba fedha za mauzo, msukule hata ukiona, hautakuwa na uwezo wa kuzuia wizi huo.
Basi, nilipomaliza kula nilimpa bakuli yule aliyeniletea chakula, akapokea kisha akaondoka huku akimng’ong’a yule muuzaji ambaye naye hakuwa na hili wala lile.
Niliokota kipande cha karatasi nikajifuta mikono kisha nikakiachia, kikaanguka chini. Yule muuzaje alishtuka kwa karatasi hiyo kuanguka lakini hakufanya kitu, akaangalia juu kwenye feni akaamini ndilo lilisababisha kuanguka kwa karatasi hiyo lakini hakutaka kujua ilianguka kutokea wapi.
Nilikwenda kukaa pembeni kidogo jirani na mlango wa uani ili nipumzike kabla ya kuanza tena kazi ya kuita wateja.
Baada ya muda nilisimama, nikaanza tena kuita kwa staili ile ile ya kuinua mikono na kufanya ishara ya kuita ambayo kila mmoja wenu anaijua.
Nilifanya shughuli hiyo hadi saa kumi na mbili jioni alipokuja yule mzee kunichukua. Huyu mzee nilivyomjua alikuwa wakala, yaani kazi yake kubwa ni kuwatawanya misukule kwa wenye maduka wanaohitaji kwa malipo maalum ya fedha za kawaida. Hii ipo hata sasa, wapo wamiliki wa maduka ambao hawana misukule, kwa hiyo wanatafuta watu wanaomiliki misukule na kuongea nao kisha wakishapatana ndiyo inakuwa kama vile.
Hata hivyo, mmiliki wa duka anatakiwa aue mtu wake wa karibu ndiyo awe msukule, hii huleta faida kubwa kama una biashara kuliko kutumia misukule ya kukodi.
Kisheria, namaanisha mfumo wa kuua mtu wa karibu ili awe msukule, inatakiwa unayemuua awe yule aliyekukaa sana moyoni. Kama ni watoto, unatakiwa uchague unayempenda kuliko wote, ama mke, mume, baba au mama.
Basi, nje ya duka nilikuta misukule wengine kama tisa, wakiwemo ambao tuko wote kule kambini. Mnaweza kujiuliza nilijuaje wale ni misukule baada tu ya kutoka kwenye duka. Ni kwamba, hakuna msukule unaovaa nguo tofauti na shuka jeupe kwa kujifunga lubega. Pia, mashuka hayo huwa machafu sana kwa mwonekano.
Kingine, misukule ni myeusi kutokana na kuishi katika mazingira machafu, kutopaka mafuta na kutegemea uji ambao ni mchanganyiko wa unga na maji tu bila kupitia jikoni.
Nywele za misukule lazima ziwe ndefu na za kujisokota kwa sababu baada ya kuoga hakuna kuchana, unadhani hapo nini kitafuata?
Basi, tuliondoka wote, lakini si kwenda moja kwa moja kambini, kwani yule mzee aliwapitia misukule wengine ambao nao aliwatawanya katika maduka mbalimbali.
Kuna sehemu tulipita nikamwona mzee mmoja jirani na nyumbani kwangu, anaitwa Masakila, nikawaambia wenzangu kwa ishara kwamba namjua yule, wakakataa, nikaminya vidole viwili vya mkono wa kulia kisha nikavibetua, vikalia taa...
ROBO YA WATU DAR NI MISUKULE -13
NYWELE za misukule lazima ziwe ndefu na za kujisokota kwa sababu baada ya kuoga hakuna kuchana, unadhani hapo nini kitafuata?Basi, tuliondoka wote, lakini sikwenda moja kwa moja kambini, kwani yule mzee aliwapitia misukule wengine ambao nao awali aliwatawanya katika maduka mbalimbali.
Kuna sehemu tulipita nikamwona mzee mmoja jirani na nyumbani kwangu, anaitwa Masakila, nikawaambia wenzangu kwa ishara kwamba namjua yule, wakakataa, nikaminya vidole viwili vya mkono wa kulia kisha nikavibetua, vikalia taa...
SASA ENDELEA…
Mzee Masakila alishtuka na kugeuka kuangalia tulipokuwa tumesimama. Kule kugeuka nikawaambia wenzangu mmeona kwa ishara ya mikono. Wakaamini.
Tulitoka eneo lile na kwenda kuwapitia misukule wengine waliokuwa sehemu mbalimbali za katikati ya jiji. Si rahisi kuamini kuwa, wapo misukule waliokuwa kando ya Bahari ya Hindi maeneo ya Posta ya zamani wakifanya shughuli mbalimbali za kijamii. Walipochukuliwa wote, tulirudishwa kwenye maskani yetu.
Hapa nataka kusema kwamba, katikati ya jiji kuna misukule wengi ambao wapo kwa ajili ya kufanya kazi za watu, hasa biashara ndogo ndogo kama kuuza maji, juisi, vocha na pipi ambazo ni za kubeba mkononi.
Unaweza ukawa umeshanunua bidhaa kwa hawa misukule lakini bila kujijua. Ila kwa ishara ambazo ziko hapa utajua kuwa siku moja uliwahi kumuungisha msukule.
Ukiachilia mbali na ile dalili ya misukule wanaouza kahawa, hawa wana ishara au dalili nyingine kabisa. Ukiwa kwa miguu au kwenye basi, huja mpaka dirishani na kukukimbizia boksi lenye bidhaa, lakini sasa kama umewahi kuona kwa mwenzako au wewe mwenyewe kushuhudia unanunua kitu, halafu ukisharudishiwa chenji mbele ya safari unakuwa hujui ilipo, ujue ulifanya biashara na msukule.
Pia, misukule hawa wana tabia ya kuonesha ufundi mkubwa wawapo kazini kwani linaweza kuja gari nyuma kwa mwendo kasi, ukajua anagongwa, lakini atakavyolikwepa wewe mwenyewe hutaamini.
Kifupi wawapo kazini wamekuwa ni wa kupitia au kuashiria ajali ajali tu, mara waruke na kukwepa pikipiki, mara wapigiwe honi na madereva wanaokimbiza magari, lakini cha ajabu sasa, hakuna dereva atakayewapigia honi kisha akachanganya na kutukana matusi kama watu wengine wa kawaida.
Basi, usiku wa siku hiyo ulikuwa wa kipekee kwani tukiwa tumelala, alikuja mwanaume mmoja na kutuamsha, kisha akasema kuwa kila aliye na kucha hatakiwi kuzikata kwani imebainika kwamba wapo wanaokata kucha kwa kutumia meno.
Kumbe bwana, kila mtu duniani ana kazi yake na ujuzi wa kitu anachokijua yeye. Ni kwamba, misukule huwa haitakiwi kuwa na kucha fupi kwani zinawapa uwezo na ujuaji.
Yaani, msukule unapokuwa na kucha fupi unaweza kutoroka kutoka kwa bosi wake au bosi wake anaweza kukosa uwezo wa kumkontroo. Ndiyo maana sifa kubwa ya msukule ni kuwa na kucha ndefu sana zinazokaribia njiti ya kiberiti.
Basi, yule mtu akatutaka wote tusimame ili kukaguliwa kila mkono na kucha zake. Mimi nilibahatika kwani licha ya kutokatwa ulimi, lakini pia kucha zangu sikuwahi kuzikata iwe kwa meno au kwa njia nyingine yoyote.
Sasa nikawa najiuliza, wale watakaokutwa na kucha fupi kwamba wamezikata watachukuliwa hatua gani? Nikasema moyoni ngoja nitaona hapo hapo.
Baada ya ukaguzi kumkuta msukule wa saba, wa nane akabainika amekuwa akikata kucha kwa meno, akachukuliwa na kupelekwa mahali pengine. Mpaka zoezi linakwisha, misukule waliobainika kukata kucha walikuwa wanne.
Wote walipelekwa kwenye chumba kimoja lakini hatukujua walichotendewa huko zaidi ya sisi kuamriwa tulale ili tuwahi kuamka eti kuna safari ya kwenda Kariakoo.
***
Ilikuwa asubuhi ya saa mbili na nusu ndipo tulipoanza safari ya kwenda Kariakoo, mkuu wa msafara wetu alikuwa mbele kama kawaida huku kila wakati akisimama pembeni na kuangalia usalama wetu.
Kabla sijaendelea mbele ya safari niseme ambalo sikuwahi kulifanyia kazi hata siku moja. Mpaka leo sijajua kama ni mimi tu au hata misukule wenzangu, ni kwamba nilikuwa nawaza nyumbani kwangu kama kawaida, namuwaza mke wangu, namuwaza mwanangu.
Lakini linapofika suala la hisia za kimapenzi, sikuwa nazo hata chembe. Nadhani ni eneo ambalo wachukuaji wa misukule hukimbilia kulifanyia kazi kwa sababu za kuogopa mimba maana tulikuwa wanawake kwa wanaume na kama si kuidhibiti hali hiyo kuna watoto wangekuwa wanazaliwa na misukule, sijui ingekuwa vipi maana kwenye maskani tulikuwa tunalala bila kujali mwanamke wapi, mwanaume wapi.
Kariakoo tulifikia kwenye kituo cha mafuta cha Msimbazi, tulisimama kwa dakika kumi na mkuu wetu, kwenye saa tatu akaja mzee mmoja wa Kiarabu akaongea na mkuu wetu kisha akaja kutuangalia sisi kama anayetukagua ili kujua tunaweza kukifanya alichotuitia au la!
“Lakini hawa ni wengi, mimi nataka nusu yake,” alisema yule Mwarabu. Pale tulikuwa kama kumi na tano.
“Sasa wengine nitawapeleka wapi muda huu, wenzao wengine kule wameshapangiwa majukumu,” alisema mkuu wetu.
ROBO YA WATU DAR NI MISUKULE-16
Mimi nilikimbia mpaka kwenye jengo moja ambalo nje kuna bustani kubwa, lakini hapaishi watu. Pembeni ya bustani palikuwa na bomba la maji, nikaenda kukaa pembeni ya bomba hilo huku nikihema kwa kasi.ENDELEA SASA…
Mara, mzee mmoja alikuja na kunikuta pale, akashtuka kwa hali niliyokuwa nayo na kuniuliza kulikoni?
Nilimsimulia kila kitu, nikamwambia ilivyotokea hadi kifo changu na maisha yangu nikiwa katika misukule.
Yule mzee alinichukua, akanipeleka kwake huku njiani akiwaambia watu mimi ni mgonjwa ameniokota, wengine walimpa pole.
Nilikaa kwa yule mzee kwa muda wa siku tatu, akaninunulia nguo, akanipeleka hospitali, siku hiyo ya tatu akanipandisha boti kurudi Dar huku akiniambia nimshukuru Mungu kwa bahati niliyoipata ya kuishi katikati ya misukule huku nikiwa sijakatwa ulimi kwani ningekatwa nisingekuwa na uwezo wa kuonekana kirahisi na kurudi duniani.
Nilitua Bandari ya Dar es Salaam saa kumi na mbili na nusu jioni. Nakumbuka ilikuwa siku ya Alhamisi. Nikapanda daladala hadi nyumbani kwangu ambapo wakati kigizagiza kinaingia, nikasimama nje ya mlango na kubisha hodi, akaja mke wangu.
Kwanza alianguka na kupoteza fahamu, ikabidi nimbebe hadi chumbani ambako nilimuweka kwenye kitanda na kuanza kumpepea. Alipopata fahamu, akataka kupiga kelele, nikamshika na kumzuia.
Nilimweleza kwa upole hali ilivyonitokea mwanzo mwisho na jinsi nilivyookotwa Zanzibar baada ya mkuu wa misukule kushtukia maisha yangu ya kuwa na wao bila kukatwa ulimi.
Awali mke wangu alionesha dalili ya kutoniamini, akaniomba akamwite mjumbe. Mjumbe alikuja akiwa ameongoza na wazee watatu na vijana wanne, walionesha dalili za kuja kwenye shari.
Waliniuliza maswali mengi na kwa muda mrefu hadi wakaanza kukubaliana na mimi. Lakini mjumbe akamuuliza mke wangu:
“Wewe mama si ulisema tangu kifo cha mumeo ulikuwa unahangaika kwa waganga ili mumeo arudi?”
Mke wangu akamjibu ndiyo mzee. Mjumbe akamuuuliza:
“Sasa ulitaka arudi kwa njia gani?”
Mke wangu akaja kunikumbatia, wale watu wakakaa sana na mimi wakiniuliza mambo mbalimbali kuhusu misukule, mwisho wake waliondoka wakisema watarudi asubuhi.
Huo ndiyo mwisho wa maisha ya mimi kuwa msukule, bahati yangu ilikuwa moja tu, kutokatwa ulimi, basi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni