Saturday, December 1, 2012
IKIMBIE ZINAA
Je! Unaamini ya kuwa Mungu
anaweza kusema na watu kwa njia ya ndoto? Najua ni rahisi kuamini kuwa Mungu
alisema na watu zamani kwa njia ya ndoto kama
tunavyosoma katika Biblia; lakini je! Unaamini ya kuwa Mungu anasema na watu
kwa njia ya ndoto siku hizi? Najua kuna watu wanaoamini na wengine hawaamini.
Sijui wewe uko upande gani. Lakini nataka nikueleze hivi; Kufuatana na Biblia
kuna ndoto za aina tatu; (a) Kuna ndoto kutoka kwa Mungu. Soma kitabu cha
Hesabu 12:6, na Yoeli 2:28. (b) Kuna ndoto zinakuja kwa sababu ya shughuli
nyingi. Soma kitabu cha Mhubiri 5:3. (c) Kuna ndoto za uongo zinazotoka kwa
shetani aliye baba wa uongo. Soma kitabu cha Yeremia 23:52 na Yohana 8:44.
Unaweza kutofautisha kwa namna gani tofauti iliyopo kati ya hizi ndoto? Na
utajuaje kuwa ndoto uliyoiota imetoka kwa Mungu? Kila ndoto lazima ipimwe na
Neno la Mungu. Ikiwa imetoka kwa Mungu, ni lazima utakuta neno la Mungu ambalo
linaeleza maana yake. Mara nyingine ndoto toka kwa Mungu huja kama fumbo;
lakini Roho Mtakatifu ajuaye kuyafumbua mafumbo ya Mungu (1 Wakorintho
2:10,11), atalifunua fumbo hilo kwa kukuonyesha neno la Mungu linalofanana na
ndoto hiyo. Si busara kuzikubali ndoto zote unazoota bila ya kuzipima katika
Neno la Mungu. Na pia si busara kuzikataa ndoto zote bila kuzipima katika Neno
la Mungu. Nimeona nianze kwa kukueleza haya kwa kuwa chanzo cha kuandika kitabu
hiki, ni ujumbe wa Mungu ulionijia kwa njia ya ndoto. Ndoto yenyewe ilikuwa
hivi: Niliona katika ndoto mtu mmoja mkristo, tena aliyeokoka akifanya mambo ya
zinaa bila hata kuogopa. Na wakati nilipokuwa nikimtazama na kusikitika,
nikasikia sauti toka juu yangu ikisema; “ NITACHUKULIANA MPAKA LINI NA MWANADAMU
AFANYAYE MAMBO YA JINSI HIYO?” Baada ya kusikia maneno hayo nikaamka. Wakati
huo ulikuwa ni alfajiri, na ndoto hiyo ilinipa maswali na masononeko mengi
moyoni mwangu. Na niliamua kumshirikisha mke wangu Diana juu ya ndoto hiyo. Mke
wangu akaniuliza; “ Maana yake nini ndoto hiyo?” Nilipotaka kufungua kinywa ili
nimjibu uchungu mzito ulijaa moyoni mwangu, nikasikia kuugua rohoni, na mara
nikaanza kulia! Unaweza ukaniuliza; “Mwakasege kwa nini ndoto ikulize machozi?”
Hili ni swali zuri. Hata mimi nilijiuliza kwa nini nitoe machozi kwa ajili ya
ndoto. Lakini baada ya kulifuatilia jambo hili katika maombi na katika neno la
Mungu nilielewa sababu yake. Je! Unafahamu matokeo ya Mungu kusema
“Nitachukuliana mpaka lini na mwanadamu afanyaye mambo ya jinsi hiyo?” Ukisikia
maneno ya jinsi hii ujue Mungu amekasirika na kuna maangamizo mbele. Hebu na
tulifuatilie jambo hili katika biblia ili tulione uzito wake. Nuhu na Gharika.
Ni vizuri ukumbuke ya kuwa gharika ilitokea wakati wa Nuhu kwa sababu ya zinaa.
“Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa
kwao, wana wa Mungu waliona hao binti za wanadamu – ni wazuri; WKAJITWALIA WAKE
WO WOTE WALIOWACHAGUA. Bwana akasema, ROHO YANGU HAITASHINDANA NA MWANADAMU
MILELE, kwa kuwa yeye ni nyama; basi siku zake zitakuwa mia na ishirini. Nao
Wanefili walikuwako duniani siku zile, tena baada ya hayo, wana wa Mungu
WALIPOINGIA kwa binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu
hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA AKAONA YA KUWA MAOVU YA MWANADAMU NI
MAKUBWA DUNIANI NA KWAMBA KILA KUSUDI ANALOWAZA MOYONI MWAKE NI BAYA TU SIKU
ZOTE. BWANA AKAGHAIRI KWA KUWA AMEMFANYA MWANADAMU DUNIANI, AKAHUZUNIKA MOYONI.
Bwana akasema, Nitamfutilia usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambulisho
na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu
akapata neema machoni pa Bwana.” (Mwanzo 6:1-8) Ukiendelea kufuatilia habari
hii katika Biblia utaona ya kuwa baada ya gharika ya maji walibaki watu nane
tu! Wanadamu wengine wote waliangamia kwa sababu ya nini? – Zinaa! Sodoma na
Gomora Wasomaji wa Biblia wanafahamu kabisa ya kuwa miji ya Sodoma na Gomora
iliteketezwa kwa moto baada ya Mungu kuihukumu kwa sababu ya uasherati uliokuwa
ukifanyika ndani yake. Soma Mwanzo 19:4-25. Na pia katika kitabu cha Yuda 1:7
tunasoma hivi: - “Kama vile Sodoma na Gomara, na miji iliyokuwa kando kando,
waliofuata UASHERATI kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili
yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.”
Ikiwa Mungu aliwatenda hivi watu wa Sodoma na Gomora, ni kitu gani kinamfanya
mwanadamu wa siku hizi adhani ya kuwa Mungu amebadilika juu ya kuadhibu wale
wote wafanyao uasherati? Katika miji hiyo miwili ni watu watatu tu waliobaki –
Lutu na watoto wake wawili! Wanadamu wengine waliokuwa katika miji hiyo
waliteketezwa kwa sababu ya nini – Zinaa! Kuhani Eli na watoto wake. “Basi Eli
alikuwa mzee sana, naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda
Waisraeli; na jinsi WALIVYOLALA NA WANAWAKE waliokuwa wakitumika mlangoni pa
hema ya kukutania.” (1Samweli 2:22) Hata baada ya baba yao kuwaonya
hawakusikia, na matokeo yake ni:- 1. Watoto hao wawili, Hofni na Finehasi
walikufa wote siku moja; 2. Wana wa Israeli walipigwa na adui zao Wafilisti na
Sanduku la agano likatekwa; 3. Kuhani Eli alikufa. Yote haya yalitokea katika
taifa ambamo watoto wawili wa kiongozi waliuwa wakifanya mambo ya Zinaa bila
hata kujali maonyo. Je! Bado unajiuliza kwa nini nilitoa machozi baada ya
kusikia sauti ya Mungu katika ndoto ikisema “Nitachukuliana mpaka lini na
mwanadamu afanyaye mambo ya jinsi hiyo?” Siku za Mwisho. “Lakini ufahamu neno
hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari. Maana watu watakuwa
wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi,
wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi…….Kwa maana
katika hao wamo wale WAJIINGIZAYO KATIKA NYUMBA ZA WATU, NA KUCHUKUA MATEKA
WANAWAKE WAJINGA WENYE MIZIGO YA DHAMBI, waliochukuliwa na tamaa za namna
nyingi. (2 Timotheo 3:1,26). Je! Siku hizi wanawake hawatekwi mateka na wanaume
ili wafanye mambo ya zinaa? Vishawishi vimekuwa vingi, na wanawake wengi
wameanguka katika mitego hiyo ya kupenda fedha na anasa, na mwisho wake ni
kufanya uzinifu. Kwa nini wanaume wengi wamekosa akili juu ya jambo hili. Ni
kitu gani kimewapofusha macho wasione ya kuwa uzinifu ni mbaya? Biblia inasema;
“Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; afanya jambo litakalomangamiza
nafsi yake.” (Mithali 6:32) Ni dhahiri ya kwamba palipo na zinaa pana
uharibufu, na wengi wanaangamia. Na nataka nikuambie ya kuwa Roho Mtakatifu
akikuwekea mzigo huo ndani yako na kuliona jambo hili jinsi linavyomhunish
Mungu, hakika hutatulia; na hapana budi macho yako yatajaa machozi juu ya
kizazi hiki kinachojiangamiza chenyewe kwa sababu ya zinaa. Sababu ya mambo
haya kuandikwa. Mambo haya hayakuandikwa kwa bahati mbaya, wala si kwa ajili ya
kuonyesha historia ya watu Fulani tu. Bali yaliandikwa kwa kusudi maalumu na
muhimu. “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili
KUTUONYA SISI, tuliofikiriwa na miisho ya zamnai – Kwa hiyo anayejidhania kuwa
amesimama na aangalie asianguke.” (1 Wakorintho 10:11,12) Na mimi nimependa
kuyaonyesha wazi ili tujue tunapozungumza juu ya zinaa, Bwana Mungu anakuwa na
mawazo gani juu yake. Nafahamu si mara kwa mara hata katika mahubiri na
mafundisho, jambo hili huguswa kwa undani. Lakini naona umefika muda wa
kulichambua jambo hili kwa undani zaidi. Hali ilivyo sasa. Mtu mmoja aliniuliza
“Je, mtu aliyeokoka anaweza kufanya mambo ya uasherati – je, anaweza kuzini?”
Nikamwambia, “Mtu aliyeokoka hatakiwi kufanya mambo ya uasherati, kwa kuwa
kufanya hivyo ni dhambi, lakini asiposimama katika Kristo sawasawa anaweza
kuzini.” Halafu huyo mtu akaendelea kuuliza, “Je, Unamfahamu Fulani? (Akamtaja
jina lake). “Ndiyo namfahamu.” Mimi nilimjibu, na nikaendelea kusema; - “ kuwa
ni mtumishi wa Mungu, ingawa sijamwona muda mrefu umepita sasa”. Ndipo akasema,
“Unafahamu ya kuwa alianguka na akazini na msichana Fulani (akamtaja jina lake)
ambaye pia ameokoka, na sasa yule msichana amezaa?” Mimi nilishangaa na
kushutushwa na habari hizo. Nikamuuliza “Unasema kweli ndivyo ilivyotokea?”
Akasema, “Ndiyo” Ndipo Roho wa Mungu aliponikumbusha ndoto ile aliyonipa.
Katika ujumbe ule wa ndoto, Mungu alinionyesha mkristo aliyeokoka akifanya
mambo ya uasherati. Kwa mtu asiyeokoka siwezi kushangaa akifanya uzinzi, kwa
kuwa bado yuko gizani, na yuko chini ya mkuu wa giza, ibilisi – kwa hiyo
anaweza kufanya lo lote lile. Ndiyo maana mtu anaweza kusema yeye ni mkristo,
na huku anazini mara kwa mara. Mkristo wa kweli aliyeokoka hatakiwi kuzini,
wala kushindwa na dhambi. Kwa nini? Kwa kuwa ndani yake ametengwa mbali na
dhambi, na amepewa ushindi juu ya dhambi. Ushindi dhidi ya dhambi Uhusiano wako
na dhambi unakuwaje baada ya kuokoka, na kufanyika kiumbe kipya ndani ya
Kristo? Watu wengi wakiisha-okoka, huwa bado wanasumbuliwa na kuanguka katika
dhambi mara kwa mara, na hasa katika zinaa. Na hii inatokea kwa kuwa hawapati
mafundisho ya kutosha ya neno la Mungu juu ya jinsi wanavyotakiwa kuenenda
katika maisha mapya waliyopita. Kaini aliambiwaje na Mungu? Bwana alimwambia
hivi; “ kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko,
inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa UISHINDE” (Mwanzo
4:7) Na ndivyo ilivyo hata sasa. Bado tumo ulimwenguni humu, ingawa aliyezaliwa
mara ya pili yeye si wa ulimwengu huu (Yohana 17:16). Lakini kwa kuwa bado tumo
katika ulimwengu uliojaa dhambi inayotutamani kila siku, na tusije tukajisahau.
Inatupasa tuishinde. Yanenaje maandiko? Imeandikwa katika kitabu cha (Warumi
6:12-14) “Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu, ipatikanayo na mauti,
hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za
dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai baada ya
kufa, na viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi, bali jitoeni wenyewe
kwa Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha
za haki. Kwa maana DHAMBI HAITA WATAWALA NINYI, kwa sababu hamuwi chini ya
sheria, bali chini ya neema”. Ikiwa tunaambiwa ya kuwa “Dhambi haitawala ninyi
…….” inakuwaje basi wengine wanatawaliwa nayo? Inakuwaje mtu wa Mungu,
aliyepakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu aanguke katika zinaa? Kitu gani
kinampofusha macho ya rohoni? Je! Ni halali kwa mtu anayekaa ndani ya Kristo
kutenda dhambi? Yanenaje maandiko? “Kila akaaye ndani yake (Yesu Kristo)
HATENDI DHAMBI; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtamua….atendaye
dhambi ni wa ibilisi; kwa kuwa ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi
hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.” (1 Yohana
3:6,8) Je! Unaona maneno haya yalivyoandikwa kwa ajili yetu? Sidhani kama
unapenda tena kuwa Ibilisi kwa kuwa “Apendaye dhambi ni wa Ibilisi” Kwa hiyo ni
muhimu ujilinde usitende dhambi. Tena imeandikwa: “Kila mtu aliyezaliwa na
Mungu hatendi dhambi, kwa sababu UZAO WAKE WAKAA NDANI YAKE; WALA HAWEZI
KUTENDA DHAMBI KWA SABABU AMEZALIWA KUTOKANA NA MUNGU.” (1 Yohana 3:9) Ikiwa
umezaliwa mara ya pili kwa Roho wa Mungu, ujue hakika UZAO WA MUNGU unakaa
ndani yako. Na uzao huu wa uungu ni Mtakatifu, na unakaa ndani yake bila
kutangatanga unakuwezesha kuishi bila kutenda dhambi. Je! Si jambo la
kumshukuru Mungu hilo. Si kwamba anatuambia tusitende dhambi bila kutupa njia
ya kutusaidia. Anajua sisi wenyewe hatuwezi kuishinda dhambi, BALI YEYE AKIKAA
NDANI YETU NA SISI NDANI YAKE TUNAWEZA KUISHI KATIKA USHINDI DHIDI YA DHAMBI NA
MITEGO YAKE YOTE. Tena imeandikwa; “Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na
Mungu HATENDI DHAMBI; bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA, wala yule mwovu
HAMGUSI.” (1 Yohana 5:18) Ee, mtu wa Mungu, jilinde basi kwa kuwa umezaliwa na
Mungu, kwa nini tamaa ya uasherati ikusonge? Je?! umesahau ni uzao wa namna
gani ulio ndani yako? Ni kweli kwamba mtu akitenda dhambi na akatubu, Bwana
atamsamehe, (1 Yohana 1:9). Lakini hatutakiwi kutenda dhambi. Ndiyo maana
imeandika; “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba MSITENDE DHAMBI”….
(1 Yohana 2:1) Sasa naona unaweza kuelewa kwa nini inashtusha na kusikitisha
unaposikia mtu wa Mungu ameanguka katika dhambi ya zinaa. Ikiwa maisha ya
wokovu yatakuwa ni ya kuanguka na kusimama, halafu tena kuanguka na kusimama
mara kwa mara; basi ina maana ya kuwa ushindi wa kutosha haukupatikana pale
msalabani. Lakini nataka nikuambie hivi, ushindi kamili ulipatikana pale
msalabani bila kubakiza kitu! Ndiyo sababu Yesu Kristo alikuwa na ujasiri wa
kusema ‘IMEKWISHA’ pale msalabani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni